Haijawahi kutokea vikwazo, vitimbi uchaguzi mdogo

Mkurugenzi wa Opareshi na Mafunzo Chadema, Benson Kigaila akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam . Picha na Anthony Siame 

Muktasari:

Sababu nyingine ni zile za kawaida za mgombea kufariki.


Dar/Mikoani. Linaweza kuwa tatizo la vyama vya siasa, hasa vya upinzani au tatizo la wasimamizi wa uchaguzi; lakini kilicho dhahiri ni kutawala kwa maamuzi na vitimbi.

Mgombea kutoweka na kuzima simu; muhuri wa chama kufichwa na baadaye muhusika kujivua uanachama; mgombea kutuhumiwa kwa mauaji hadi mgombea kupewa mtihani wa kuandika neno “zinjathropus” ni baadhi ya matukio yaliyotawala uchaguzi mdogo wa madiwani na wabunge safari hii.

Hata baadhi ya sababu za kurudia uchaguzi huo Agosti 12 zinafuata mkondo huo. Baadhi ya nafazi zimekuwa wazi baada ya waliokuwa wanazishikilia kujivua uanachama na kujiunga na chama kingine na halafu kuomba tena na kupitishwa kutetea viti vyao.

Sababu nyingine ni zile za kawaida za mgombea kufariki.

Jana, mgombea udiwani wa Kata ya Mpona (Chadema), Iskaka Mloge alienguliwa baada ya msimamizi wa uchaguzi kujiridhisha na mapingamizi yaliyowekwa na mgombea wa CCM, Michael Siwingwa kuwa Mloge si raia.

Pingamizi dhidi yake pia lilihusu taarifa alizotoa kuwa ni mkulima, lakini msimamizi akajiridhisha kuwa ni mfanyabiashara, na alijiridhisha kuwa kada huyo wa Chadema aliandika kwenye fomu namba ambayo si yake.

Mpaka sasa wagombea 12 wa udiwani kupitia chama hicho kikuu cha upinzani nchini wameenguliwa, wakidaiwa kukosa sifa hizo na wengine kushindwa kurudisha fomu au kujibu pingamizi dhidi yao.

Hilo limewafanya wagombea udiwani wa CCM  katika zaidi ya kata 20 kupita bila kupingwa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi mdogo katika kata 77 na moja ya Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Chadema kuchezewa rafu na taratibu za wagombea wenye sifa, mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Athuman Kihami alisema ni vigumu kutolea ufafanuzi masuala ambayo hayajapelekwa rasmi ofisi ya tume hiyo. 

“Kama yataletwa yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Walioenguliwa Arusha

Juzi, mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Aman Golugwa  alisema wamebakiwa na wagombea tisa tu baada ya kumi na moja kuenguliwa.

Alisema katika Jiji la Arusha, ambalo linajulikana kama ngome ya upinzani hasa Chadema,  uchaguzi utakuwa katika kata nne, pia kuna wagombea wawili wa kata ya Osunyai na Kaloleni wamewekeza mapingamizi na tayari yamejibiwa.

“Huu uchaguzi utakuwa mgumu sana,” alisema Golugwa.

“Tayari tumelalamika Tume ya Taifa ya Uchaguzi na  polisi. Kuna sehemu mgombea wetu aliambiwa kuandika jina la zinjanthropus  na alipokosea akaondolewa eti hajui kusoma na kuandika. Mwingine amenyang’anywa fomu mlangoni.”

Katibu mwenezi wa CCM wa mkoa, Shaaban Mdoe alisema chama hicho kimejiandaa kurejesha kata zote akidai kuwa wagombea wengi wa Chadema wamejitoa baada ya kubaini hawatoshi katika nafasi walizoomba.

“Kuna mapingamizi yamewekwa kihalali na wengine wamejitoa baada ya kubaini hawajui kusoma na kuandika,” alisema.

Kwa upande wao, wasimamizi wa uchaguzi walisema taratibu zote zimefuatwa katika uchaguzi, ikiwamo baadhi ya wagombea kuenguliwa kwa kukosa sifa.

Msimamizi uchaguzi wa Wilaya ya Longido ambako kata tatu zinafanya uchaguzi, Jumaa Mhina alisema mgombea mmoja wa Chadema katika kata ya Alang’atadapash, Isaya Laizer hakurejesha fomu.

Mhina alisema katika Kata ya Kamwanga,  Sakimba Alais (Chadema) pia aliwekewa pingamizi kwa tuhuma za kutojua kusoma.

Pia msimamizi Jimbo la Ngorongoro, Raphael Siumbu alisema wagombea wanne wa CCM wamepita bila kupingwa.

Siumbu alisema katika kata moja ya Alaitole mgombea mmoja alijitoa baada ya kushindwa kujibu pingamizi dhidi yake kuwa hajui kusoma wala kuandika.

Katika Halmashauri ya Monduli, msimamizi wa uchaguzi, Steven Ulaya alisema kati ya kata sita, wagombea wawili wa CCM wamepita bila kupingwa.

Katika uchaguzi huo, CCM ilipitisha wagombea wote 19 waliokuwa madiwani kwa tiketi ya Chadema, lakini wakajiuzulu na kujiunga na chama tawala.

Mpaka sasa CCM imeshinda katika kata 19, zikiwamo 11 za jiji la Arusha, tano za Halmashauri ya Tunduma, kata ya Mpona katika Halmashauri ya Songwe, mbili za Serengeti, mara na ya Kimara jijini Dar es Salaam.

Mchakato uanze upya

Wakati huo huo, Chadema imeitaka NEC kusitisha uchaguzi kwenye baadhi ya maeneo na kuanza upya mchakato wa kupata wagombea ili kila mtu mwenye haki apate nafasi hiyo.

Maeneo yaliyobainishwa na chama hicho ni Tunduma kwenye kata tano ambako wagombea udiwani walinyimwa fomu. Kwingine ni Arusha ambako mgombea katika kata ya Terati alinyang’anywa fomu mbele ya msimamizi wa uchaguzi.

Pia, Iringa ambako chama hicho kinadai wasimamizi katika kata mbili za Gangilonga na Kilosa walikataa kupokea fomu za wagombea wao, jambo ambalo  Chadema wanadai linawatengenezea CCM mazingira ya ushindi.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, mkurugenzi wa kampeni na uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi alisema wameiandikia barua Tume kuitaka kusitisha uchaguzi katika kata wanazodai hawajatendewa haki.

“Pamoja na rufaa tulizopeleka Tume, kuna mambo tunayoitaka iyazingatie. Kwanza ni Tume itendee haki rufaa zote zilizopelekwa ili wagombea waweze kurudi kufanya kampeni,” alisema Munisi.

Mkurugenzi huyo pia alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi zake bila kuingilia uchaguzi kwenye Jimbo la Buyungu na kwingineko.

“Kuna kata 18 ambazo wagombea wa Chadema wameenguliwa. Mpaka sasa kuna maeneo watu wetu wamekataliwa rufaa zao. Kwa mfano Rombo. Tumeandika malalamiko yetu kwa Tume,” amesema Munisi.

Lakini mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Songwe, Elias Newala aliliambia Mwananchi jana kwamba ofisi yake ilifuata taratibu zote za uchaguzi kumuengua Mloge.

“Wagombea wote walichukua fomu na wote wakarejesha vizuri tu na baada ya hapo ukatolewa muda wa kuwasilisha mapingamizi na CCM wakaleta pingamizi dhidi ya mgombea wa Chadema ambayo kimsingi Tume iliridhika nayo,” alisema Newala.

Lakini hakueleza pingamizi lilihusu nini.

CUF na fomu za uchaguzi

Kadhia hiyo pia imeikumba CUF, ambayo imeingia katika uchaguzi mdogo ikiwa katika makundi mawili.

Upande unaomuunga mkono Profesa Ibrahimu Lipumba umesema hadi sasa wagombea wake katika kata sita wameenguliwa kwa sababu mbalimbali, hasa kukosea kujaza fomu.

Mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma wa chama hicho, Abdul Kambaya amezitaja kata hizo kuwa ni Kolo (Kondoa)  Nachingwea (Ruangwa) na Kitaya (Nanyamba).

Nyingine ni Tangazo na Nanguruwe (Mtwara Vijijini ) na Kimara Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kambaya alisema chama hicho kitatoa taarifa kamili baada ya kukusanya taarifa zote.

“Inaonyesha kuna maelekezo tu,” alisema Kambaya.

“Hakuna hoja za kisheria. Ni uamuzi tu wasimamizi wa uchaguzi  wa ngazi ya kata.”

Kambaya alisema hakuna ukweli kuwa wagombea wanakosea kujaza fomu bali wahusika wameitafuta hiyo kama hoja.

“Hebu jiulize hivi mwaka gani wagombea wa CCM wamewahi kuenguliwa kwa mapingamizi? Ina maana wao hawakosei?” alihoji Kambaya.

Imeandikwa na Bakari Kiango na Ibrahim Yamola (Dar), Godfrey Kahango (Mbeya) na Musa Juma (Arusha).