Haki za binadamu wapaza sauti

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa .

Muktasari:

  • Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo.

Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umeitaka   Polisi mkoani Arusha kuwafikisha mahakamani wanachama wake wanne inaowashikilia kwa siku 12 sasa.

Mtandao huo umedai kuwa watu saba wilayani Longido wanatuhumiwa kutoa taarifa kwa mwanahabari wa Sweden, Susana Nurduland ambaye anafuatilia kwa karibu migogoro ya ardhi wilayani humo.

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema uendeshaji wa madai hayo umegubikwa na upendeleo wa wazi, kinyume na matakwa ya sheria za nchi kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai.

Aliwataja walionyimwa dhamana kuwa ni Samwel Nangiria, Supuk Olemaoi, Clinton Kairung na Yohana Mako wakati walioachiwa ni mbunge wa zamani wa Ngorongoro, Mathew ole Timan, Diwani wa Ololosokwani, Yanick Ndina Timan na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mundoros, Joshua Makko.