VIDEO: Hakielimu yakosoa ujenzi wa madarasa, mabweni kwa miezi miwili

Muktasari:

  • Juni 17, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo alitangaza uamuzi huo uliolenga kuwawezesha wanafunzi 21,808 waliokosa nafasi za kujiunga na kidato cha tano kupata fursa hiyo.

Dar es Salaam. Shirika la Hakielimu limeonyesha wasiwasi katika utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kujenga vyumba vya madarasa 478 na mabweni 269 ndani ya miezi miwili.

Juni 17, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo alitangaza uamuzi huo uliolenga kuwawezesha wanafunzi 21,808 waliokosa nafasi za kujiunga na kidato cha tano kupata fursa hiyo.

Akizungumza na wanahabari, mkurugenzi mtendaji wa Hakielimu, Dk John Kallage alisema muda ambao Serikali imetoa ni mfupi kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo kwa ufanisi.

Alisema endapo hakutakuwa na usimamizi wa karibu upo uwezekano wa kazi hiyo ikafanyika katika ubora hafifu.

“Kufanikisha ujenzi wa madarasa 478 na mabweni 269 kwa ubora ndani ya miezi miwili ni ngumu kwakweli, hasa ikizingatiwa hatua za awali za kuandaa ardhi, wataalam na mambo mengine zilikuwa hazijafanywa,”alisema.

Alisema wasiwasi mwingine umeonekana katika uwekwaji wa mazingira bora ya kujifunza na kufundishia kwa wanafunzi hao watakaojengewa madarasa.

“Serikali inapaswa kuangalia kuwa hao wanafunzi wakiongezeka mahitaji sio madarasa na mabweni pekee kuna suala la vitabu, walimu, vitanda, madawati, meza sasa hatufahamu haya yote yanawekwa vipi na bajeti ambayo imeelezwa ni Sh29 bilioni pekee,”

Dk Kallage pia aliweka msisitizo kwa Serikali kutoa kiasi hicho cha fedha na kukitumia kama ilivyohaidi.

Kwa mujibu wa Dk Kallage katika miaka ya karibuni kumekuwa na tofauti kati ya mipango ya serikali na bajeti inayotolewa katika miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Kuhusu hatua hiyo ya dharura Dk Kallage alisema ongezeko la ufaulu wa wanafunzi lilionekana tangu Februari hivyo Serikali ingeamua kuchukua hatua hizo mapema wanafunzi hao wasingelazimika kusubiri miezi miwili.

“Hatua zingechukuliwa mapema miundombinu hii ingeshakamilika na hawa wanafunzi wangeanza masomo na wenzao,” alisema.

“Tunachoomba kifanyike kwa hawa wanafunzi wanaisubiri miundombinu ni muhimu Serikali ikaweka mpango mahsusi wa kuwafidia muda wao wa masomo uliopotea ili kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na kuchelewa huko.”