Hakimu amsweka rumande shahidi kwa kosa la uchelewaji

Muktasari:

Malale anatuhumiwa kukutwa na fedha bandia zenye thamani ya Sh290, 000.


Misungwi, Askari wa kitengo cha upelelezi kituo cha Misungwi wilayani Misungwi, Mwanza, PC Tumaini Kiweru amewekwa mahabusu kwa saa mbili, kwa kosa la kuchelewa mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo Erick Marley, aliamuru PC Kiweru kuwekwa chini ya ulinzi leo Julai 11 kwa kosa la kuichelewesha mahakama,  ilipokuwa inamsubiri kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Mahojiano kati ya Hakimu Marley na PC Kiweru mahakamani hapo yalikuwa hivi:

Hakimu Marley: Wewe ni nani?

Shahidi: PC Tumaini, ni shahidi wa kesi hii.

 Hakimu Marley: Ulikuwa wapi?

Shahidi:  Niliitwa na Occid,Hakimu.

Hakimu Marley: Nini?

Shahidi: niliitwa na OCCID.

 Hakimu Marley: Ukadharau wito wa Mahakama, basi utakaa chini ya ulinzi na watuhumiwa wengine.

PC Tumaini alikuwa shahidi wa tatu kwa  upande wa mashtaka katika kesi  inayomkabili mkazi wa Igoma, Mwanza, Moja Malale(35).

Malale anatuhumiwa kukutwa na fedha bandia zenye thamani ya Sh290, 000.

Baada ya shahidi kuwekwa rumande, mahakama iliahirishwa kwa saa mbili ili shahidi   huyo atumikie adhabu na baadaye iliendelea.

PC Tumaini akiongozwa na mwendesha mashitaka wa polisi Ramsoney Salehe ,aliapa na kuanza kutoa ushahidi.

Awali mwendesha mashtaka wa polisi Ramsoney Salehe alimsomea hati ya mashtaka   Malale  na kuieleza mahakama kuwa  mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 10 kakijiji cha Nyamatala, kwenye mnada wa upili,  akiwa na noti hizo bandia