Hakimu azikataa hoja za vigogo Chadema

Viongozi wa Chadema  wakiwa wamekaa (mbele) katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Viongozi hao wanakabiliwa na shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Asema amekalia benchi miaka 22 hajawahi kukataliwa na mtu yeyote

Dar es Salaam. Hakimu mkazi mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri amekataa kujitoa kuiendesha kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na kusema maombi yao hayana mashiko.

Mashauri alitoa uamuzi huo jana mbele ya wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya na mawakili wa Serikali, Faraja Nchimbi, Dk Zainab Mango, Paul Kadushi, Kishenyi Mutalemwa na Wankyo Simon.

Akitoa uamuzi huo, Mashauri alisema maombi ya utetezi ya kutaka ajitoe kuiendesha kesi hiyo yanataka kuchelewesha haki.

Akichambua baadhi ya hoja walizozitoa washtakiwa hao ikiwamo sharti la wao kuripoti polisi ni adhabu tosha, alisema sababu hiyo haina msingi kwa sababu ni takwa la kisheria.

Kuhusu kutokuwa na imani kwa sababu ya maombi yao yote, Mashauri alisema hilo halina maana kwa kuwa pande zote zimekuwa zikipewa nafasi ya kusikilizwa.

Alisema yeye amekalia benchi kwa miaka 22 na hajawahi kuombwa na yeyote ajitoe, hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Julai 18 kusubiri maombi yaliyopo Mahakama Kuu.

Julai 2, Mbowe na wenzake wanane walipeleka maombi wakitaka kubadilishiwa hakimu anayesimamia kesi hiyo kwa madai kuwa, hawana imani naye.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 likiwamo la kuchochea ghasia, kukaidi amri ya polisi, uchochezi na uasi. Wanadaiwa kufanya makosa hayo, Februari 16 wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana.

Katika tukio hilo, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline alipigwa risasi akiwa kwenye daladala eneo la Kinondoni, Mkwajuni.

Wengine katika kesi hiyo ni katibu mkuu, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu mkuu bara na Zanzibar, John Mnyika na Salum Mwalimu, wabunge Esther Bulaya (Bunda mjini), Esther Matiko (Tarime mjini), Peter Msigwa (Iringa mjini), John Heche (Tarime vijijini) na Halima Mdee (Kawe).

Kesi ya Haonga, Mbozi

Wakati hayo yakijiri Dar es Salam, mjini Mbozi mkoani Songwe, hukumu ya kesi inayomkabili mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga na wenzake, imeahirishwa hadi Agosti 10 huku hakimu akitoa sababu tatu za kuahirisha hukumu hiyo.

Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mbozi, Nemes Chami alisema kutokana na majukumu mengi aliyonayo hukumu hiyo haijakamilika.

Pia, kutokana na unyeti wa shauri lenyewe; tatu kesi hiyo ina makabrasha mengi hivyo anahitaji muda wa kutosha kuyapitia na ndiyo maana aliiahirisha.

Haonga na wenzake Wilfredy Mwalusanya ambaye ni katibu wake na Mashaka Mwampashi, wanakabiliwa na makosa ya kufanya fujo na kuvuruga mkutano wa baraza la uchaguzi la mji mdogo wa Mlowo; kuwazuia askari kutekeleza majukumu yao.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 28 mwaka jana mjini Mlowo-Mbozi.