Hakuna aliye salama, Mawaziri 9 wamefyekwa

Dar es Salaam. Nani atafuata? ni swali ambalo mawaziri kumi na moja na manaibu 15 wanaweza kuwa wanajiuliza baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa mawaziri wawili kati ya 19 waliokuwemo katika baraza lake la kwanza.

Na hasa wakikumbuka hotuba yake ya mjini Tabora kuwa hatakoma kutengua uteuzi wa wateule wake iwapo ataona wanamkwamisha.

“Anayekaa njiani anatumbuliwa. Na kutumbua tutaendelea kutumbua wala siogopi,” alisema Julai mwaka jana wakati akihutubia wananchi mjini Tabora.

Juzi, ametengua uteuzi wa Dk Charles Tizeba, aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Charles Mwijage (Viwanda na Biashara), uamuzi ambao umefanya idadi ya mawaziri aliotengua uteuzi wao kufikia nusu ya aliowatangaza Desemba 10, 2015.

Katika baraza la kwanza lililotangazwa Desemba 10 mwaka 2015 lililokuwa na wizara 18, Magufuli aliteua mawaziri 19 na manaibu wao 15, lakini hadi sasa wamesalia kumi na moja na manaibu 10.

Kati ya manaibu hao wa baraza la kwanza, watano walipandishwa na kuwa mawaziri kamili baada ya Rais Magufuli kutangaza mabadiliko madogo ya mawaziri kwa nyakati tofauti.

Mawaziri hao 11 waliosalia kwenye baraza hilo ni Angellah Kairuki (Madini), January Makamba (Muungano na Mazingira), Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Profesa Makame Mbarawa (Maji), Profesa Philip Mpango (Fedha na Mipango) na Dk Harrison Mwakyembe (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo).

Pia yumo Dk Augustine Mahiga (Mambo ya Nje), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), William Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia) na Ummy Mwalimu (Afya).

Mawaziri waliofukuzwa kazi au kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ni Dk Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani), Profesa Sospter Muhongo (Nishati na Madini), Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani) na Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii).

Wengine ni Nape Nnauye (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwekezaji) na George Simbachawene (Tamisemi).

Manaibu waliokumbana na fagio au kuachwa ni Edwin Ngonyani, Ramo Makani, Dk Susan Kolimba na Annastazia Wambura.

Katika baraza la mwanzo yumo Dk Abdallah Posi, ambaye alilazimika kujiuzulu unaibu waziri baada ya kuteuliwa kuwa balozi, wakati kukiwa na mjadala kuwa idadi ya wabunge wanaume ambao ni wateule wa rais imezidi kiwango cha uwiano wa kijinsia kilichowekwa kikatiba.

Katika kipindi hicho tangu baraza la kwanza litangazwe, manaibu watano walipandishwa na kuwa mawaziri kamili. Walioteuliwa Desemba 10, 2015 kuwa manaibu na baadaye kupandishwa ni Seleman Jaffo, Luhaga Mpina, Dk Medard Kalemani, Dk Hamis Kigwangalla na Isaack Kamwelwe.

Manaibu mawaziri watano waliosailia tangu walipoteuliwa Desemba 10, 2015 ingawa wengine walihamishwa wizara ni; Anthony Mavunde, Willam Ole Nasha, Dk Ashantu Kijaji, Angelina Mabula na Stella Manyanya.

Baraza hilo aliliteua ikiwa ni mwezi mmoja tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015. Siku hiyo alisema alichelewa kutangaza timu yake kwa kuwa alikuwa anaandaa liwe dogo.

“Nimepunguza baraza ili liwe dogo na ukipunguza baraza automatically na makatibu wakuu wanapungua. Tunasave (tunaokoa) kiasi gani, mabilioni mangapi ili ziweze kwenda kwa wananchi yakafanye kazi kama tulivyoahidi,” Magufuli aliwaambia waandishi wa habari siku hiyo.

“Ukichukua hao mawaziri na manaibu waliokuwepo katika awamu iliyopita, ukichukua mishahara yao na matumizi yao mengine, tutakuwa tume save hela fulani kwa mwezi mzima na nafikiri ni mabilioni ya kutosha.

“Tutayaangalia ni kiasi gani ili tuweze kuyatumia kwenye mambo muhimu zaidi ya maendeleo ya nchi yetu. Tutakuwa na baraza dogo na hili litatusaidia kupunguza matumizi na litatusaidia kufanya kazi kwa ufanisi.”

Mwaka 2005 akitangaza baraza lake la kwanza, Jakaya Kikwete aliteua mawaziri 29 na manaibu 31, idadi ambayo ilikuwa kubwa kulinganisha na marais waliopita, lakini alipofanya mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, alilipunguza baada ya kuteua mawaziri 26 na manaibu 21.

Suala sio kuwafukuza, kuwateua

Akizungumzia ‘tenguatengua’ hizo, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa, Gaudence Mpangala alisema suala si idadi ya mawaziri, hofu inayotokana na mawaziri kufukuzwa kila mara na hivyo mawaziri kushindwa kutumia kwa ufanisi uzoefu wanaoupata.

“Nadhani huu ndio utawala uliofukuza mawaziri wengi kwa muda mfupi wa miaka mitatu,” alisema Profesa Mpangala.

“Sijui kama ni udhaifu au wana makosa, ila kama mtu amejenga uzoefu katika wizara aliyopo na kuweka mikakati, ghafla tu unamuondoa na kuleta wengine wapya, hapo kunakuwa na shida,” alisema Profesa Mpangala ambaye alisema wakurugenzi pia wanaathiriwa na tenguatengua hiyo..