Hali ya uchumi nchini yawaibua wabunge

Muktasari:

  • Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Bunge za Bajeti; Uwekezaji na Mitaji na ile ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa mwaka 2017 juzi, wabunge hao walisema hali hiyo inajidhihirisha kutokana na takwimu zilizotolewa na taasisi kadhaa ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hali ya uchumi nchini imewaibua wabunge wakitaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kubadili sera za Taifa ili kuchochea ukuaji wake.

Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Bunge za Bajeti; Uwekezaji na Mitaji na ile ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa mwaka 2017 juzi, wabunge hao walisema hali hiyo inajidhihirisha kutokana na takwimu zilizotolewa na taasisi kadhaa ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema umefika wakati kwa Wizara ya Fedha na Mipango kukubali kubadili sera za kibajeti.

Alinukuu takwimu za BoT za mwaka 2011 hadi Desemba 2017 kuwa Pato la Taifa kwa mwaka 2011 lilikua kwa asilimia 7.8 lakini sasa inakisia litakua kwa asilimia 6.8.

Mbunge huyo alisema pia mzunguko wa fedha umeshuka kutoka asilimia 22 kwa mwaka 2011 hadi asilimia 1.8 mwaka huu na ukuaji wa usafirishaji nje wa mazao hasa ya kilimo kilichoajiri watu wengi, pia umeshuka.

Bashe alisema ongezeko la idadi ya watu ni asilimia zaidi ya mbili lakini ukuaji wa kilimo ni asilimia 0.04 , hivyo hakuna muunganiko.

Alisema takwimu hizo zinatoa jibu kuwa sera za Taifa hazitoi kichocheo cha ukuaji wa biashara na uchumi katika nchi.

“Hili jambo tunaweza kusema humu ndani ya Bunge lisiufurahishe upande wa Serikali lakini tuna jukumu la kuwaambia ukweli na ni muhimu Wizara ya Fedha na Mipango ikakubali kwamba sera za Wizara ya Fedha si rafiki katika kuchochea uchumi wetu kukua,” alisema Bashe na kuongeza kuwa taarifa iliyopelekwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Msajili wa Hazina inaonyesha mapato ya BoT yanayotokana na biashara yameshuka kwa asilimia 63.

Alimshauri Waziri wa Fedha atakapowasilisha bungeni mpango wake wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/19 awasilishe na muundo wa namna gani Tanzania inawekeza katika uzalishaji.

Akijibu suala hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema baadhi ya hatua chache zinazochukuliwa kukuza uchumi ndizo zenye matukio ya moja kwa moja lakini nyingi zinachukua muda kuona matokeo.

Alisema Serikali inachofanya sasa ni kutumia fedha nyingi za bajeti kuongeza au kuchachua miundombinu na kulipa madai ambayo yamehakikiwa.

Alisema hatua nyingine wanazochukua ni kushusha kodi katika maeneo ambayo wanahamasisha kama Taifa.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alisema katika taarifa ya wepesi wa kufanya biashara kwa viashiria vya nchi kumi na moja ambavyo vimetolewa, Tanzania imeporomoka kwa viashiria saba.

Alichambua kipengele cha upitishaji wa shehena bandarini akisema takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya 180 kati ya 190 ingawa bandari ndiyo mahali pekee kunakoiingizia nchi fedha nyingi.

Alisema hali ni mbaya na katika Bandari ya Dar es Salaam kwani kuna mlundikano wa makontena ambayo yamezuiwa kwa sababu ya mgongano.

“Watu wa TBS (Shirika la Viwango) wanasema hawawezi kuruhusu makontena yatoke mpaka wapate certification kutoka TRA (Mamlaka ya Mapato). TRA wanasema hawawezi kutoa mizigo hadi wapate certification kutoka TBS unaweza kuona contradiction (mgongano) ya watu wanaofanya kazi katika Serikali moja, wanavyoshindwa kufanya kazi kwa pamoja,” alisema.

Alisema kwa kuonyesha kuwa uchumi umeendelea kuyumba, Serikali imefunga baadhi ya benki kwa utetezi kuwa wigo wake ni mdogo.

“Ukiangalia zile benki 12, benki nane zinatakiwa kufungwa kwa sababu zina - run (zinajiendesha) chini ya faida. Nilipenda Serikali iangalie hili,” alisema.

Alisema mzunguko wa fedha umepungua kwa asilimia 45 na watu hawawezi kuagiza vitu lakini bado Serikali imekuwa ikisema kuwa fedha zipo.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema katika bajeti zilizopita, kambi ya upinzani ilisema kitendo cha kuondoa kodi ya majengo kwenye halmashauri kwenda TRA ni kuzifanya zisiendelee.

Alisema Waziri wa Fedha na Mipango anavunja sheria kwa makusudi katika suala la kodi ya majengo kwa sababu Serikali imeshindwa kukusanya kodi na kuirejesha katika halmashauri kama sheria inavyomtaka.

“Mnatudanganya kuwa mmefanikiwa nitakupa mfano mmoja wa halmashauri yetu (Kinondoni) 2016/17 walikusanya Sh10 bilioni wakiwa na Halmashauri ya Ubungo tukawa tunapanga kuongeza mkapata tamaa mkachukua… Sasa hivi miezi sita imepita hamjaleta hata senti tano,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema wanarejesha fedha walizozikusanya kutoka na kodi ya majengo kama sheria inavyotaka.

“Tukisema kule Geita wakusanye kodi ibaki kulekule na kule Mererani wakusanye inayotokana na Tanzanite ibaki kulekule hatutakuwa na Taifa.”

Alisema bajeti ya maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa ni Sh14.2 bilioni na wamepeleka Sh11 bilioni ambayo ni asilimia 70 kwa miezi sita lakini kodi waliyokusanya ya majengo ni Sh10 bilioni.

“Nimuulize Kinondoni walikusanya Sh10 bilioni lakini ni mradi gani wamefanya kwa kodi ya majengo? Tusilidanganye Taifa hili na tukalikatakata, ”alisema.

Alisema Mdee analidanganya Bunge na kwamba mwaka 2014/15 Kinondoni ilikusanya Sh5 bilioni lakini Serikali ilipeleka zaidi ya Sh9 bilioni kwa ajili ya maendeleo.

Ufisadi katika vitambulisho

Katika mchango mwingine, Silinde alisema mradi wa hati za kusafiria umekuwa ukitekelezwa kwa gharama za dola 40 milioni za Marekani.

“Kuna taarifa nimezipata kuwa mradi huo ulikuwa na thamani ya dola 16 milioni sawa na pauni 11 milioni. Kuna taarifa kuna kampuni ambayo ilishapewa memorandum of understanding (makubaliano ya awali) ambayo haikusainiwa hadi dakika ya mwisho lakini mwisho wa siku ilipewa kampuni ya HID,” alisema.

Alisema kampuni HID ambayo imepewa kazi hiyo wakati haijawahi kufanya kazi ya mradi wa hati za kusafiria mahali popote na imekuwa ikitengeneza kadi za ku-swap.

Silinde alisema kampuni hiyo imeingia ubia na watu ambao walikuwa Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) wakati uliopita.

“Kwa hiyo mwenyekiti ufisadi bado upo na uchumi umeendelea kuyumba lakini watu wameendelea kufichaficha tu kwa namna fulani, kama tunapinga ufisadi lazima hatua ichukuliwe,” alisema.

Alisema taarifa walizonazo za ndani katika mradi wa hati za kusafiria, kuna ufisadi wa kutisha katika jambo hilo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alisema ufisadi hauna nafasi kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo alisema iko macho.

“Taarifa alizosema si hizo, mwanzoni wakati hatua zilipokuwa zikichukuliwa kabla ya Serikali kuingilia kati ukubwa wa mradi ule na dola zilizokuwa zikihitajika kutumika ni 192 milioni,” alisema.

Alisema sehemu za mradi zilikuwa nne na gharama za dola 57.8 milioni za Marekani zitatumika kukamilisha mradi huo wa hati za kusafiria za kielektroniki.