Halmashauri 10 zenye kiwango cha juu malaria hizi hapa

Muktasari:

  • Halmashauri  10 za wilaya na miji zenye kiwango cha juu cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria na 14 zenye kiwango cha chini ya asilimia moja zimetajwa leo Jumatatu Oktoba 22, 2018

Dar es Salaam. Halmashauri  10 za wilaya na miji zenye kiwango cha juu cha maambukizi ya malaria na 14 zenye kiwango cha chini ya asilimia moja zimetajwa leo Jumatatu Oktoba 22, 2018.

Akizungumza wakati akizindua awamu ya pili ya matokeo ya utafiti wa viashiria vya Malaria Tanzania (TMIS) 2017, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema licha ya maambukizi hayo kupungua kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015/17 mpaka kufikia asilimia 7.3, changamoto ipo katika wilaya 10.

Amesema wilaya zenye kiwango kikubwa cha malaria ni Kakonko asilimia 30.8, Kasulu (27.6), Kibondo (25.8), Uvinza (25.4), Kigoma (25.1), Buhigwe (24), Geita (22.4), Nanyamba (19.5), Muleba (19.4) na Mtwara (19.1).

Amezitaja wilaya zenye maambukizi ya kiwango cha chini ya asilimia moja kuwa ni Mbulu TC, Mbulu DC, Hanang, Hai, Siha, Moshi MC, Mwanga, Kondoa TC, Meru DC, Arusha CC, Monduli, Ngorongoro na Rombo DC.

Ummy amesema lengo la Serikali ni kufikia kiwango cha chini ya asilimia moja ufikapo 2020 na kutokomeza kabisa malaria ifikapo mwaka 2030.

Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC) Dk Albina Chuwa akizungumzia  utafiti huo amesema uzinduzi wa kwanza ulionyesha kiwango cha maambukizi  kimepungua karibu na nusu,  yaani asilimia 7.3 kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015.

Hata hivyo,  amesema takwimu za maambukizi ya malaria katika ngazi ya halmashauri imefanyika kwa mara ya kwanza tangu NBS ianze kufanya tafiti hizo kuanzia mwaka 2000.

“Ukiangalia takwimu za hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017 ambao umeendelea kukua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 7.0 mwaka 2016 tafsiri ya haraka ni kwamba baadhi ya shughuli za kiuchumi kama vile za afya na huduma za jamii zimechangia kwenye ukuaji huo,” amesema Dk Chuwa.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Salma Kikwete amesema huu ni wakati muafaka kwa halmashauri zenye kiwango cha juu cha maambukizi kuangalia uwezekano wa kununua viuatilifu katika kiwanda cha Kibaha ili kutokomeza kabisa malaria katika maeneo yao.