Kibaha yaomba msaada ujenzi wa hospitali

Tatu Selemani

Muktasari:

Wanataka kupata hospitali mpya ya wilaya

 

Kibaha. Mrundikano wa wagonjwa katika Kituo cha Afya Mlandizi umeiibua Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kuwasilisha ombi la Sh4.2 bilioni serikalini kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Halmashauri hiyo tayari imetenga Sh121 milioni katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ili kuanza kazi hiyo mara moja.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Tatu Selemani amesema hayo leo Februari 24, 2018 katika  kikao cha bajeti ya halmashauri kilichohudhuriwa na  madiwani 14, watendaji na  viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.

Selemani amesema wamefikia hatua ya kuomba fedha hizo kutokana na changamoto wanazopata katika utoaji wa huduma kwenye Kituo cha Afya Mlandizi hasa ya mrundikano mkubwa wa wagonjwa kuliko uwezo wa kituo hicho ambayo ndio sasa inatumika kama ya wilaya.

Sababu nyingine ya kuomba ombi maalumu wakati huu ni kuwepo ongezeko kubwa la wahitaji huduma za afya huko Mlandizi, ujenzi wa viwanda, wananchi katika mamlaka ya mji mdogo wa Mlandizi na pia wanahudunia wengine wa maeneo jirani kama Bagamoyo, Chalinze na Kibaha mjini.

"Tunaiomba Serikali kuu Sh4.2 bilioni za ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya, halmashauri tayari tumetenga Sh121 milioni za kazi hiyo, maana pale kituo cha afya Mlandizi  tumeelemewa kwani tunahudumia na jirani zetu,” amesema.

“Vilevile kuna ongezeko la viwanda, idadi ya wakazi imekuwa kubwa mjini, majeruhi wa ajali barabara ya Morogoro wanatuhusu na mengine mengi."

Kuhusu Kituo cha Afya Mlandizi kupanuliwa kuwa hospitali ya wilaya, amesema wamepokea mapendekezo na ushauri mbalimbali kuwa huduma zitaendelea kutolewa hapo, lakini bado eneo hilo ni dogo na hivyo wameamua katika bajeti ya mwaka huu wajenge nyingine itakayokuwa na eneo kubwa na majengo makubwa ya kutosha kulingana na kasi ya ongezeko la wakazi.