Halmashauri tano za Ukawa hatarini

Muktasari:

  • Hamahama hiyo imeiathiri zaidi Chadema ambayo ilishinda kata nyingi kulinganisha na vyama vingine vya upinzani.

Halmashauri tano zilizo chini ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ziko hatarini kuchukuliwa na CCM kutokana na wimbi la madiwani kujivua uanachama na kuhamia chama hicho tawala.

Hamahama hiyo imeiathiri zaidi Chadema ambayo ilishinda kata nyingi kulinganisha na vyama vingine vya upinzani.

Halmashauri hizo ni Arusha, Arumeru, Hai, Siha na Iringa ambazo madiwani wake, hasa kutoka Chadema wametimkia CCM kutokana na sababu tofauti, kubwa ikiwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli.

Tangu hamahama hiyo inayohusisha madiwani na wabunge ilipoanza, CCM imeonekana kunufaika zaidi kuliko Chadema kwa kuwa hata uchaguzi unaporudiwa chama tawala kinaibuka mshindi hivyo kuongeza idadi ya madiwani.

CCM ilinufaika katika uchaguzi mdogo wa kata 43 ilipotwaa kata 42, huku Chadema ikipata moja mkoani Mbeya. Hata hivyo, ushindi huo ulichangiwa zaidi na tangazo la kujitoa la Ukawa kutokana na madai ya wagombea kukamatwa, mawakala kuzuiwa kuingia vituoni na vurugu. Vyama hivyo pia vimesusia uchaguzi mdogo wa majimbo matatu uliofanyika jana, vikitaka mkutano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kujadili kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo wa madiwani.

Tayari zaidi ya madiwani 21 wa upinzani hususan Chadema wamejiuzulu na kuhamia CCM na hakuna dalili za hali hiyo kutulia kutokana na madiwani zaidi kuendelea kuachia ngazi.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara(, John Mnyika anaona wimbi hilo halitaendelea.

“Haiwezekani halmashauri zote hizo wakaweza kuchukua madiwani kwa kiwango cha kuzichukua. Tunaendelea kudhibiti mikakati yao michafu,” alisema Mnyika ambaye chama chake kilipokea makada kadhaa kutoka CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga alisema kikubwa wanachokipigania ni kuleta maendeleo kwa wananchi na hilo la kuhamahama haliwasumbui.

Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Baraza la Madiwani la Iringa Mjini lilikuwa na wajumbe 28, kati yao madiwani wa kuchaguliwa 18, viti maalumu sita na wabunge wanne.

Katika idadi hiyo Chadema ilishinda kata 14 na kupata viti vitano vya udiwani wa viti maalumu.

Hadi sasa madiwani tisa wamejiuzulu, kati yao sita ni wa kuchaguliwa na watatu wa viti maalumu na tayari NEC imejaza nafasi mbili kati ya hizo na hivyo Chadema inabaki na wajumbe 14 katika baraza la madiwnai hilo huku CCM ikiongeza madiwani kutoka saba hadi tisa baada ya kushinda kata mbili zilizokuwa wazi.

Ikiwa NEC itarejesha jina jingine kuziba nafasi ya diwani wa viti maalumu iliyo wazi na CCM kushinda kata nne zilizowazi za Mwangata, Mkwawa, Kwakilosa na Ruaha itafikisha wajumbe 13 katika baraza hilo na Chadema 15 hivyo kuwa na tofauti ya wajumbe wa wawili.

Ikiwa madiwani wawili watajiuzulu ndani ya kipindi hiki na uchaguzi kufanyika kisha kuipa ushindi CCM, chama hicho kitakuwa na wajumbe 15 huku Chadema ikiwa na wajumbe 13 jambo linaloweza kuchangia meya wa manispaa hiyo kupoteza nguvu za kulinda nafasi yake iwapo baraza hilo litapoteza imani naye.

“Huwezi kumzuia mtu kuhama na kama wakiwa CCM wengi ni kweli tunaweza kupoteza halmashauri,” alisema mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alipoulizwa kuhusu wimbi hilo.

“Lakini sisi si tatizo kwa kuwa wananchi wanataka ajira, uchumi na kutatua matatizo yao si kununua madiwani. CCM na Serikali inatakiwa kuwekeza katika kutatua matatizo ya wananchi na si kutaka kuchukua halmashauri.

“Tunarudia uchaguzi wa udiwani katika kata sita, zaidi ya Sh200 milioni (zitatumika), fedha hizi zingeelekezwa katika kutatua kero za wananchi, lakini sasa tunaziteketeza kwa uzembe tu wa watu.”

Meya wa manispaa hiyo, Alex Kimbe alisema inauma na ni sawa na mtu kuvuliwa nguo, lakini akasisitiza kuwa hata kama watajiuzulu wote yeye atabaki kuwa diwani na atawatumikia wananchi waliomchagua.

Halmashauri za Arusha Mjini, Arumeru mkoani Arusha, Hai na Siha mkoani Kilimanjaro zimepoteza jumla ya madiwani 15 ambao walitimkia CCM huku chama hicho tawala kikichukua kata zilizorudia uchaguzi na huenda ikafanya hivyo katika kata nyingine.

“Chochote kinaweza kutokea katika utaratibu huu, lakini siyo tishio kubwa sana la mageuzi ya kweli kwetu,” alisema mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

“Nafikiri CCM wamethibitisha pasipo shaka udogo wa nguvu zao katika demokrasia huru. Tuko njiani kufanya maamuzi ya mioyo ya kulinda haki na uhuru wa demokrasia katika nchi yetu.”

Lema anaamini kuna uungwaji mkono mkubwa wa mageuzi dhidi ya chama tawala kwa sababu kuu ya tabia za CCM zilivyo sasa.

“Wakati Waisraeli wanaondoka utumwani Misri haikuwa kazi rahisi ila walifanikiwa kwa msaada wa Mungu,” alisema Lema anayeongoza jimbo hilo kwa muhula wa pili.

“Nafikiri pengine sisi tunaweza kushindwa lakini Mungu je? Aliyetupa macho kweli asiweze kuona mambo yote haya yanayoendelea? Haki ya kweli haiwezi kushindwa na jeshi lolote lile, wakati ni jibu.”

Mbali na madiwani ambao inajikusanyia, CCM ina nafasi kubwa ya kuliongoza jimbo la Longido lililokuwa chini ya mbunge wa Chadema, Onesmo Ole Nangole ambaye alivuliwa ubunge na Mahakama.

Majimbo ya Kinondoni na Siha ambayo uchaguzi wake utafanyika Februari 17 nayo huenda yakatwaliwa na CCM baada ya waliokuwa wabunge wake ambao wote walikuwa wa upinzani kujiuzulu kwa sababu ileile ya kumuunga mkono Rais.

Waliojiondoa ni Dk Godwin Mollel wa Siha-Chadema na Maulid Mtulia wa Kinondoni- CUF. Baada ya kuhamia CCM, wote wawili wamepitishwa na chama hicho tawala kugombea tena nafasi walizojivua.