Halmashauri za Geita, GGM wavurugana

Muktasari:

  • Madiwani katika kikao cha pamoja wameazimia kukata mawasiliano na GGM kushinikiza kulipwa fedha za ushuru wa huduma.

Geita. Madiwani wa halmashauri mbili za Wilaya ya Geita wametangaza mgogoro na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Kikao cha kutangaza mgogoro huo leo Jumatano kimehudhuriwa na madiwani wa halmashauri hizo, mwakilishi wa GGM, wakurugenzi wa halmashauri zote mbili na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi.

Madiwani hao wametangaza kuzuia magari ya mgodi kwa kufunga barabara na kufunga maji yanayoingia mgodini kutoka Ziwa Victoria.

Mgogoro huo unatokana na madai ya halmashauri ya kulipwa na GGM Dola 12 milioni za Marekani zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Wakizungumza kwenye kikao hicho cha pamoja, madiwani Magulu Kuzenza, Mapande Enock, Pastor Ruhusa na Ngulungu Juma wamesema kitendo cha mgodi kuwataka waende mahakamani kuhusu malipo hayo ni cha kuwadharau.

Madiwani hao wamesema fedha hizo ni haki yao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mgodi ulipaswa kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 lakini hawakulipa na badala yake walilipa Dola 200,000 kwa mwaka tangu 2004 hadi 2013 kinyume cha sheria.

Meneja mahusiano ya jamii kutoka mgodi wa GGM, Manase Ndoroma amesema kinachosababisha mgogoro kati ya pande hizo mbili ni kupingana kwa sheria ambazo zote zimetungwa na Bunge.

Amesema sheria ya madini iliwaruhusu kulipa Dola 200,000 kwa mwaka, huku sheria ya baraza la madiwani ikiwa imepitisha malipo ya asilimia 0.3 jambo linalosababisha mgogoro na suluhisho pekee ni kwenda mahakamani.

Halmashauri hizo na GGM zimekuwa kwenye mgogoro kwa zaidi ya mwezi sasa kutokana na madai ya fedha hizo.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Musukuma amesema watakata mawasiliano kati yao na mgodi hadi watakapolipwa.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kapufi amesema akiwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama atakachofanya ni kusimamia amani na kuhakikisha hakuna mali itakayoharibika kutokana na mgogoro huo.

“Siwezi kuzuia kwa kuwa kila mtu anaona yuko sawa, nitaandika barua kuwataarifu GGM wasitoe magari yao kesho kwa usalama wa mali zao hadi watakapofikia muafaka,” amesema.