Halmashauri zapewa siku saba kwenda kuchukua madawati

Muktasari:

Alisema JKT walipewa zabuni ya kutengeneza madawati 60,000 yenye thamani ya Sh3 bilioni na zaidi ya 30,000 yalikamilika katika awamu ya kwanza.

Dar er Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ametoa siku saba kwa majimbo 18 kwenda kuchukua madawati yao yaliyotengenezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kabla hawajashauri mamlaka husika kuyagawa kwa maeneo mengine yenye mahitaji. Waziri Mwinyi aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Alisema JKT walipewa zabuni ya kutengeneza madawati 60,000 yenye thamani ya Sh3 bilioni na zaidi ya 30,000 yalikamilika katika awamu ya kwanza.

Dk Mwinyi alisema matengenezo ya madawati mengine 30,000 ya awamu ya pili yatakamilika kabla ya Agosti 30, tarehe ya mwisho iliyotolewa na Rais Magufuli kukamilisha shughuli hiyo.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Kilindi, Pangani, Makambako, Ludewa, Wanging’ombe, Makete, Tunduru Kaskazini, Songwe,  Ileje, Kyela, Rungwe, Busokelo, Kwela, Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Iringa Mjini, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini.

Alisema kushindwa kwenda kuyachukua ni sawa na kukinzana na kauli ya Rais Magufuli.