Hamad atoa agizo zito kwa waganga

Muktasari:

  • Alitoa agizo hilo wakati akizindua mkoba maalumu wa vifaa vya mjamzito ambao hutolewa bila malipo kwa wajawazito wanapofika hospitalini kujifungua.

Zanzibar. Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed amewataka watendaji wa vituo vya afya kuorodhesha dawa zinazohitajika maeneo yao kwa kuwa dawa za bure kwa wagonjwa zipo za kutosha.

Alitoa agizo hilo wakati akizindua mkoba maalumu wa vifaa vya mjamzito ambao hutolewa bila malipo kwa wajawazito wanapofika hospitalini kujifungua.

Hamad alisema Serikali imepanga kuhakikisha wajawazito na wananchi wananufaika na utolewaji huduma za afya bila malipo sambamba na kupatiwa dawa kulingana na mahitaji ya mgonjwa.

Naye mkurugenzi wa kinga na elimu, Dk Fadhil Abdallah alisema idadi ya wajawazito wanaojifunguli vituo vya afya imeongezeka, ila elimu zaidi inahitajika wawe wanafika vituoni mapema.

Mwakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), Maryam Seif Hemed aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinaimarika kila mara.

Hata hivyo alitoa wito kwa Wizara ya Afya kuhakikisha inaweka mikakati ya kuvitunza vifaa tiba na kuviondosha vilivyoharibika kwenye vituo vya afya ili kulinda afya za wananchi.