Hamahama ya wanachama ACT yamtikisa Zitto

Muktasari:

  • Katika hotuba hiyo, mbunge huyo wa Kigoma Mjini aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kujiuliza maswali magumu, likiwamo la kwa nini hali hiyo inakikumba chama chao.

 Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe jana alitumia hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu kuzungumzia wimbi la kuhama kwa makada wa chama hicho na kuhoji kama kimeanza kupoteza mwelekeo.

Katika hotuba hiyo, mbunge huyo wa Kigoma Mjini aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kujiuliza maswali magumu, likiwamo la kwa nini hali hiyo inakikumba chama chao.

Makada wa chama hicho waliotimkia CCM ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliachia nafasi ya ushauri wa chama hicho baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, wakili Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga.

Katika maelezo yake alisema hamahama hiyo imezua taharuki kwenye chama hicho na kuacha maswali juu ya kinachoendelea katika siasa za Tanzania.

“Lakini ni lazima tujiulize maswali magumu sisi wenyewe na kuzungumza tukitazamana machoni je, hakuna sababu za ndani sisi wenyewe zinazokimbiza wanachama wetu? Kama zipo ni zipi? Je, ni sababu ambazo tunaweza kurekebisha na kukiimarisha chama,” alihoji.

“Kama ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu tunafanya nini ili kuzikabili je, bado sisi tunaamini katika misingi ya chama kwa mujibu wa Azimio la Tabora? Tulikuwa kundi tu tulioumizwa na vyama tulivyokuwamo na tukaamua kuunda chama kupoza hasira zetu tu na sasa hasira zimeisha hakuna sababu ya chama kuwapo.”

Alisema kati ya waanzilishi watatu wa ACT, wawili wamekikimbia na kujiunga na CCM na kufafanua kuwa jambo hilo huenda likarutubisha hoja kuwa chama hicho kilikuwa mradi wa chama tawala, kwamba mradi huo sasa hauna maana tena.

“Kwamba sasa CCM inavunja mradi wake au? Mnaweza kujiuliza mbona Chadema na CUF wanakwenda CCM labda mradi huo ulihusisha wanachama wa vyama vingine vya upinzani,” alisema.

Alihoji sababu za wanachama wa vyama vya TLP, UDP, NRA kutokimbilia CCM na kupuuza hoja kuwa vyama hivyo ni dhaifu.

“Haya maswali ni lazima tuyajibu kwa ukweli wa mioyo yetu ili kuweza kujisahihisha kama tuna makosa yetu wenyewe. Ni muhimu tujitafakari,” alisema.

Zitto alisema sababu inayotolewa na watu wote wanaoondoka upinzani kuwa wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli hazitoshi kueleza uamuzi wao na hasa wanaotoka ACT -Wazalendo.