Hapi aiagiza Takukuru kuchunguza mradi wa Sh400 milioni Malangali

Muktasari:

Ni mradi unaogharimu Sh 400 milioni ambao utahusisha ujenzi wa kituo cha Afya cha Malangali, nyumba ya mtumishi na maabara ya kisasa.

Mufindi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeagizwa kuanza mara moja uchunguzi wa mradi wa uboreshaji wa kituo cha Afya Malangali baada ya kubainika utekelezaji wake una harufu ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi ametoa agizo hilo leo Septemba 11, baada ya kukagua mradi wa ujenzi na ukarabati wa kituo cha afya cha Malangali unaogharimu S400milioni.

Amesema kuwa fedha hizo zilitolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa jengo la maabara, nyumba moja ya mtumishi pamoja na maabara ya kisasa.

Hapi amewataka viongozi wa Halmashauri kuhakikisha  wanasimamia utekelezaji wa miradi badala ya kuwaachia wahandisi.

"Nawataka viongozi wa halmashauri kuwa na utaratibu wa kufuatilia ujenzi na fedha zinazotumika na sio kuwaachia wahandisi ambao wanatumia kigezo cha ongezeko la thamani kuiibia serikali na msiwaamini wahandisi na wakibainika ni lazima wachukuliwe hatua" amesema.

Hapi amesema taasisi hiyo inatakiwa kuwachunguza kwa kina mhandisi wa Halamashauri ya Wilaya ya Mafinga, Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, pamoja na kamati ya ujenzi ya kijiji kwa kuwa wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya ujenzi huo.

Alisema kuwa fedha zilizotumika kukarabati na ujenzi Wa miundombinu hiyo haiendani na fedha halisi zilizotolewa na Serikali.

Mkuu wa Takukuru Mkoani Iringa Aidani Ndomba amesema uchunguzi wa ujenzi huo utaanza mara moja utakaojumuisha kupitia nyaraka za awali za upanuzi wa kituo hicho cha afya.