Happi awarushia madongo wapinzani

Muktasari:

Francis Mkwela mkurugenzi wa kampuni ya AFROMAP inayotekeleza upimaji wa viwanja katika eneo hilo, anasema hadi sasa wamefanikiwa kupima viwanja zaidi ya 5000.


Dar es salaam.Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amerusha madongo kwa wapinzani kuwa mtaji wao wa kutumia migogoro mbalimbali ya wananchi ikiwamo ya ardhi ‘utafilisiwa’ na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa imejikita kuimaliza.

Ameyasema hayo leo Machi 23, wakati akizindua uwekaji wa alama za mawe (beacons) kwenye viwanja vilivyopimwa katika eneo la Nyakasangwe ambalo liligubikwa na migogoro ya ardhi iliyosababisha watu 10 kuuawa mwaka 2012. 

Amesema anajisikia furaha kwa kufanikiwa kutatua mgogoro huo na kuuweka katika hali ya kuelekekea kuwa eneo lenye maendeleo kutokana na utambuzi wa mipaka kukamilikia kwa asilimia 90.

"Kwa hatua hii inaonyesha kuwa Rais alichagua mtu sahihi na siyo muuza sura kama, tunatatua hii migogoro ambayo wapinzani hutumia kama mtaji wao sasa itafika wakati watakosa cha kuzungumzia," amesema.

Mkurugenzi wa kampuni ya AFROMAP, Francis Mkwela inayotekeleza upimaji wa viwanja katika eneo hilo, amesema hadi sasa wamefanikiwa kupima viwanja zaidi ya 5,000. 

Mkwela amesema mradi wa upimaji umegawanyika katika sehemu mbili viwanja visivyo na migogoro na yenye migogoro ambavyo vinahusisha wananchi zaidi ya 3,900.