Harmorapa apiga dili na kampuni ya usafirishaji

Muktasari:

Baada ya dili hilo kutangazwa Harmorapa aliwashangaa wanaomuona chizi wakati anazidi kutengeneza mkate wa kila siku


Dar es Salaam. Kama bado unamuona Harmorapa ni kituko endelea kumuona hivyo yeye anaendelea kupiga dili zake na maisha yanamuendea.

Kauli hiyo ameitoa muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa balozi mpya wa kampuni ya usafirishaji ya Moovn.

Hamorapa ameeleza kuwa anawashangaa wanaomuangalia kama mtu asiyekuwa na akili timamu wakati yeye anafahamu anachokifanya.

"Wanaoendelea kuniona chizi shauri yao wapo watu wanaonielewa na kama mnavyoona wanataka kufanya kazi na mimi naingiza mkate wa kila siku, "

Kuhusu ubalozi alioupata Harmorapa ameeleza kuwa atafanya kazi hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moovn, Godwin Gabriel amesema kampuni yake imeamua kumchagua Harmorapa kwa kuwa ni mfano wa vijana wa kitanzania wanaojituma.

Amesema kwa kutanua wigo wa biashara yao wameona ni vyema kuwatumia vijana wa kitanzania wenye ushawishi kwenye jamii.

"Hii ni kampuni ya kizalendo na ndiyo sababu tumeamua kuwachukua vijana wa hapa hapa nchini wale wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari," alisema

Amesema kampuni hiyo inajipanga kuwa bora zaidi katika usafirishaji kwa kutumia App.

Sanjari na Harmorapa, mtangazaji Hamis Mandi 'Bdozen' pia ametangazwa kuwa balozi wa kampuni hiyo.