Friday, July 21, 2017

Hatari ya ‘password’ kwenye simu za mkononi

 

By Tumaini Mswoya, Mwananchi ; tmsowoya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zipo simulizi kadhaa za baadhi ya watu waliofanikiwa kuokoa uhai wao na wapendwa wao kwa kutoweka nywila ‘password’ kwenye simu zao za mkononi.

Hata hivyo, baadhi hupendelea kuweka nywila kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa usalama wa simu zao.

Baadhi ya watumiaji wa simu hizo na wachambuzi mbalimbali wanasema kuna uzuri na ubaya wa kuweka nywila kwenye simu ya mkononi.

Mmoja wa watumiaji wa simu, Nancy Nyalusi amesema tangu mdogo wake Hitra Nyalusi alipopata ajali mbaya ya barabarani na simu yake isiyo na nywila kutumika kwa ajili ya mawasiliano, hajawahi tena kuweka.

“Mdogo wangu aliwahi kupata ajali ya pikipiki maeneo ya Kimara, alijibamiza kichwa na akapoteza fahamu, bahati nzuri askari wa usalama barabarani alikuwa karibu, akakimbilia simu yake kisha akatafuta jina lililoandikwa mama, na kupiga,” amesema.

Mkazi mwingine wa Magomeni jijini Dar es Salam, Athman Juma amesema mkewe alipoteza uhai baada ya mwanae kushindwa kupiga simu yenye nywila kuomba msaada alipozidiwa kwa shinikizo la damu.

“Mtoto wangu wa darasa la tatu alishindwa kupiga simu ya kuomba msaada kwa sababu mke wangu aliweka ‘password’, na kibaya zaidi, geti lilikuwa limefungwa hivyo hata alipopiga kelele, nje hawakusikia,” amesema.

Mtaalamu wa Mitandao, Dk Barack Mwambeta amesema: “Kuweka password kwenye simu sio muhimu kabisa hasa kwa mtu mwaminifu. Simu hubeba vitu vingi muhimu vyenye uhusiano wa karibu wa muhusika mfano ukipata ajali na ukashindwa kujitambua, msaada wako wa kwanza wa kuwapata ndugu zako ni simu. 

-->