Hatima ya Benki ya KCBL Moshi bado kizungumkuti

Muktasari:

KNCU ilishaanza mchakato wa kuuza shamba lake la Lerongo kwa Sh5 bilioni ili kuinusuru benki hiyo isifungwe na Benki Kuu Tanzania (BoT), ifikapo Juni.

Uongozi wa Chama cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), sasa utalazimika kutafuta njia mbadala ya kuinusuru Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupiga marufuku kuuza mali za ushirika kipindi hiki kwa kuwa zinahakikiwa.

KNCU ilishaanza mchakato wa kuuza shamba lake la Lerongo kwa Sh5 bilioni ili kuinusuru benki hiyo isifungwe na Benki Kuu Tanzania (BoT), ifikapo Juni.

Chama hicho kikongwe zaidi cha ushirika barani Afrika, kinachomiliki asilimia 69 ya benki kiliamua kuuza shamba lake hilo lenye ukubwa wa ekari 581 ili kuiongezea benki hiyo mtaji kukidhi masharti ya BoT.

Kwa sasa benki hiyo ina mtaji wa Sh1.5 bilioni na ilitakiwa iongeze hadi kufikia Sh5 bilioni na KNCU ilipanga kwamba ungepatikana kwa kuuzwa kwa shamba hilo.

Uamuzi wa kuuza shamba hilo uliridhiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa KNCU wa Juni 23, 2017, ikiwa ni miezi sita kabla ya agizo la BoT kwa KCBL na benki zingine mbili la kuzitaka kuongeza mtaji.

Baada ya mkutano huo, Desemba 14, KNCU ilipokea kibali cha kuuzwa kwa shamba hilo kutoka ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini ambacho kiliwataka kukamilisha uuzaji huo ndani ya miezi minne.

Lakini jana, akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Serengeti, wilayani Serengeti juzi, Waziri Mkuu alisema ni marufuku kuuza mali za ushirika katika kipindi hiki ambacho Serikali inazihakiki na watakaobainika kuzihujumu watachukuliwa hatua.

Mara baada ya kauli hiyo ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliwaita ofisini kwake meneja mkuu wa KCBL, Joseph Kingazi na wa KNCU, Honest Temba na kuwapa maagizo hayo.

“Nimewaita na nimewapa maagizo ya Waziri Mkuu. Sisi kama Serikali hatuwezi kuruhusu kuuzwa kwa mali za ushirika. Tunataka tujue kwa nini benki ya ushirika imefikia hapo,” alisema Mghwira.

Kingazi alithibitisha kuitwa na mkuu wa mkoa na kupewa maagizo hayo na kusema KCBL ni waendeshaji hivyo wanasikiliza uamuzi wa wamiliki ambao ni KNCU.

“Athari ya benki kutoongeza mtaji wake kama BoT ilivyoagiza inajulikana. Kama mwenye benki ndio mwenye shamba na kama amenyimwa kuliuza hatuna la kusema. Sisi tunasubiri maelekezo,” alisema.

“Nimekutana na RC (mkuu wa mkoa) na amenipa hayo maagizo na hatuna jinsi tunapaswa kuyaheshimu. Ikifika mahali BoT wakisema rudishieni milango tutarudishia,” aliongeza.

Mwenyekiti wa Bodi ya KNCU, Aloyce Kitau alisema juzi jioni kuwa alipigiwa simu na kujulishwa juu ya uamuzi huo wa Serikali na kusema wanauheshimu na hawako tayari kukiuka.

Alipoulizwa kuhusu hatima ya maagizo ya BoT, alisema KCBL itabidi ifuate maagizo hayo na KNCU ambayo ni wana hisa itaendelea kufuatilia mwenendo wake katika kipindi hicho cha miezi sita.

Benki hiyo ya Ushirika, ilifunguliwa mwaka 1996 na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye siku hiyo yeye na mkewe, mama Anna Mkapa, walifungua akaunti.