VIDEO: Hatima ya Kubenea, Komu kujulikana muda wowote

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene.

Muktasari:

Hatima ya wabunge wawili wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) itajulikana muda wowote baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania


Dar es Salaam. Hatima ya wabunge wawili wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) itajulikana muda wowote baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania.

Kikao hicho cha dharura kinachofanyika leo Jumatano Oktoba 17, 2018 katika ukumbi wa Ledger Plaza katika Hoteli ya Bahari Beach kilikuwa na ajenda moja ya kuwajadili wabunge hao.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hiyo kwa kile walichoeleza ni ya kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Baada ya Komu kumaliza kuhojiwa na kumpisha Kubenea,  Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema kesho watatoa maazimio ya kikao hicho.

“Tumekuwa na kikao tangu saa tano asubuhi. Kikao hiki ni cha dharura na ajenda yake ni moja. Ni kuhusu clip (sauti) inayosambaa ikiwahusisha wabunge wetu Komu na Kubenea,” amesema Mrema.

“Tumewaita wabunge hawa ili waieleze kamati kuu nini kinaendelea. Komu ameshamaliza kuhojiwa mahojiano yanayoendelea sasa ni kati ya kamati na Kubenea.”

Amesema baada ya kikao hicho kumalizika kitatoa maazimio ambayo yatawekwa wazi, huku akibainisha kuwa kamati kuu ni chombo cha nidhamu.