Hatima ya Maua Sama, Soudy Brown bado kitendawili

Muktasari:

  • Mwanamuziki  Maua Sama, meneja wake Fadhili Kondo na mtangazaji wa Clouds, Soudy Brown wanaendelea kushikiliwa kituo kikuu cha polisi  jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya saa 84 wakituhumiwa kuharibu mali

Dar es Salaam. Mwanamuziki  Maua Sama, meneja wake Fadhili Kondo na mtangazaji wa Clouds, Soudy Brown wanaendelea kushikiliwa kituo kikuu cha polisi  jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya saa 84 wakituhumiwa kuharibu mali.

Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Septemba 20, 2018 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema wanashikiliwa kwa kosa la uharibifu wa mali kwa kurusha fedha na kuzikanyaga.

Amesema wamewakamata baada ya kuona video zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wakiwa baa wakifanya kitendo hicho ambacho ni kinyume na sheria za nchi.

Wengine wanaoshikiliwa hadi sasa ni msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, mshereheshaji Antony Luvanda, mtangazaji wa Clouds, Shafii Dauda  na watu wengine watatu.

Makene anashikiliwa baada ya kuitikia wito wa ofisi ya mkuu wa upelelezi Kanda Maalum (ZCO), kuhojiwa kuhusu uhalali na maudhui ya blog anayodaiwa kuiendesha.

Wakili wa Makene, Fredy Kihwelo amesema anaendelea kufuatilia dhamana ya mteja wake kwa kuwa ana haki kisheria ya kupewa dhamana, kutaka atafutwe baadaye.

Akizungumza na MCL Digital leo wakili wa Maua, meneja wake na Soudy, Jebra Kambole amesema wateja wake bado wanaendelea kushikiliwa na leo anaweza kufahamu nini kinaendelea.

“Ni kweli wateja wangu wanaendelea kushikiliwa na leo sijaweza kufika polisi niko mahakamani naomba nitafute mchana nitakujulisha kinachoendelea,” amesema Kambole.