VIDEO: Hatua kwa hatua kutekwa, kupatikana Mo Dewji

Muktasari:

Unaweza kusema mengi yametokea na kuzungumzwa tangu kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ Oktoba 11, 2018 hadi leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 saa nane usiku alipopatikana baada ya watekaji kumtelekeza katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam


Dar es Salaam. Oktoba 11, 2018  saa 11:30 alfajiri mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ alitekwa wakati akiwa katika Hoteli ya Colosseum Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Tangu siku hiyo hadi leo saa nane usiku Oktoba 20, 2018 alipopatikana yapo mambo mengi yameibuka kuhusu wapi alikokuwa bilionea huyo ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40.

Viongozi wamiminika hotelini

Takribani saa mbili tangu Mo Dewji kutekwa askari polisi na viongozi mbalimbali walifika katika hoteli ya Colosseum.

Baadhi ya waliojitokeza ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa pamoja na maofisa kadhaa wa usalama.

Ulinzi ulikuwa mkali katika eneo hilo wakati maofisa wa polisi wakifanya uchunguzi wa awali kwa kutumia vipimo mbalimbali.

Mambosasa ataja wahusika wa utekaji

Muda mchache baada ya kufika katika eneo la tukio,   Mambosasa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Mo Dewji alitekwa na Wazungu wawili waliokuwa katika gari aina ya Toyota Surf, kwamba kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa ndani na jingine nje ya hoteli hiyo. Alisema wahusika walikuwa wamefunika nyuso zao.

Uvumi wazagaa Dewji amepatikana

Kuanzia saa sita mchana Oktoba 11, 2018 taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo zilianza kuzagaa ikidaiwa kuwa zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda akanusha

Taarifa hizo zilikanushwa na Makonda  na kubainisha kuwa huenda waliotoa taarifa hizo walimnukuu vibaya.

Manara akamatwa na polisi

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikamatwa na polisi kutokana na tukio la kutekwa kwa Mo Dewji kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia, jambo ambalo lilidaiwa kuwa si kweli.

Manara alikamatwa Oktoba 11 jioni na kuachiwa kabla ya kukamatwa tena Oktoba 12, 2018 asubuhi.

Lugola azungumza

Jumamosi, Oktoba 13, 2018 Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alizungumza na vyombo vya habari na kubainisha kuwa polisi inaendelea na mchakato wa kumtafuta mfanyabiashara huyu.

Aliwaeleza wanahabari kuwa  wakati huo watu 20 walikuwa wakishikiliwa na polisi akataka ndani ya saa 24 watu wanaowashikilia kwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo mara baada ya kuwahoji na kubaini hawahusiki au hawana taarifa kamili waachiliwe.

Wanaoshikiliwa na polisi wafikia 26

Hadi kufikia Jumapili, Oktoba 14 idadi ya watu waliokuwa wakishikiliwa kwa mahojiano kuhusu tukio la kutekwa kwa Dewji ilifikia 26, akiwemo Manara.

Jeshi la polisi lilisema hatua hiyo ni sehemu ya kazi ya uchunguzi na baada ya kukamilisha kuwahoji taarifa zaidi ingetolewa.

Masauni na CCTV

Jumapili Oktoba 14, 2018 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali inatarajia kusambaza kamera maalum za CCTV katika miji mikubwa na baadhi ya mikoa ili kukabiliana na matukio ya uhalifu.

Sh1 bilioni kutolewa

Jumatatu mchana, Oktoba 15, 2018  familia ya Dewji ilitangaza donge nono la Sh1 bilioni kwa yoyote atakayefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo  na kwamba familia hiyo imeahidi kumlinda mtoa taarifa hizo.

Familia ilitangaza namba za simu zitakazotumika kukusanya taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea huyo.

19 waachiwa kwa dhamana

Oktoba 16, 2018 Mambosasa alisema watu 19 kati ya 26 waliokuwa wakishikiliwa na  polisi wakihusishwa na tukio la kutekwa mfanyabiashara huyo wameachiwa kwa dhamana, akiwemo Manara.

Kampuni yakanusha kufunga viwanda

Oktoba 17, Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL) ilisema inaendelea  na uzalishaji na kukanusha taarifa ya kusitisha shughuli zake  kutokana na tukio la kutekwa kwa Dewji.

Kupitia ukurasa wa Twitter, uongozi wa kampuni hiyo ulisema, “tunaendelea kusikitishwa  na tukio lililomtokea ofisa mtendaji wa kampuni yetu, Mohammed Dewji.”

“Pia, tunatoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Oktoba 20 tunasimamisha shughuli za uzalishaji katika kampuni yetu. Taarifa hiyo si ya kweli.”

Wananchi wamlilia

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo liliwagusa  maelfu ya Watanzania ambao kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii waliandika ujumbe mbalimbali wakitaka juhudi zaidi zifanyike kumpata bilionea huyo, baadhi kushangazwa siku kukatika bila kupatikana.

Polisi wabaini gari

Oktoba 19, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alizungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa gari iliyotumika kumteka mfanyabiashara huyo ilikuwa na namba za nje ya Tanzania na kutaja namba zake za usajili kuwa ni AGX404MC huku akitangaza jeshi la polisi kufanya operesheni ya kuwakamata waliomteka mfanyabiashara huyo.

Kauli ya Sirro utekwaji wa Mo yazua mjadala

Oktoba 19, baada ya Sirro kueleza hatua za uchunguzi juu ya kutekwa Mo Dewji ikiwamo kubaini gari iliyotumiwa na watekaji kuliibua mjadala mzito mtandaoni.

Wanasiasa,  wanaharakati na wananchi walihoji maswali mbalimbali kuhusu ufafanuzi huo wa Sirro wakiwemo mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

“...taratibu za gari kupita mpakani zinatia mashaka makubwa kauli ya IGP. Polisi na vyombo vya usalama nchini hutumia plate number (namba za gari) za kigeni. Ile picha ya gari sio ya CCTV. Kamanda Sirro Hapana,” amesema Zitto.

Mo apatikana

Mo Dewji amepatikana leo saa nane usiku huku Mambosasa akisema  mfanyabiashara huyo alitelekezwa kwenye Viwanja vya Gymkhana katikati ya jijini la Dar es Salaam.

Amesema polisi walipata taarifa leo saa nane usiku kuwa mfanyabiashara huyo amepatikana na watekaji walimchukua kwenye gari waliyotumia kumteka na kumtelekeza katika viwanja hivyo.

“Polisi tulipata taarifa kwamba amepatikana, watekaji walimchukua kwenye gari ile ile waliyotumia kumteka na kwenda kumtupa katika viwanja hivyo,” amesema Mambosasa.

“Tangu alivyotekwa pale hoteli ya Collesium (alfajiri ya Oktoba 11, 2018) gari ya watekaji iliondoka kasi na baada ya dakika  15 Dewji alijikuta amewekwa kwenye chumba akiwa amefunikwa  ili asiwatambue watekaji.”

Baba yake azungumza

Gullam Dewji Hussein, baba wa mfanyabiashara huyo leo Oktoba 20 amesimulia jinsi alivyompata mwanaye.

Gullam amesema alijulishwa kuwa mwanaye amepatikana akiwa katika gari ambalo lilitelekezwa katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa.

Amesema Mo Dewji baada ya kushushwa katika gari hilo alitembea kutafuta msaada wa simu.

Amebainisha kuwa baada ya kupokea simu hiyo alifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumuona mwanaye.