Hawa ndio waigizaji 10 wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani

Muktasari:

Orodha hiyo Iliyotoka hivi karibuni inamweka George Clooney katika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri wa dola 239 milioni. 

Ukiachilia mbali taarifa za wanamichezo wanaolipwa mkwanja mrefu zinazomuweka mbele mwanadada Serena Williams kwa upande wa wanawake na Floyd Meyweather kwa upande wa wanaume, hii hapa orodha ya waigizaji wa 10 wanaolipwa fedha nyingi. Jarida la Forbes lilitoa orodha ya wacheza sinema wanaoweka kibindoni kiasi kikubwa cha fedha huku George Clooney akitamba kwa mara ya kwanza katika orodha hiyo.

Orodha hiyo Iliyotoka hivi karibuni inamweka George Clooney katika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri wa dola 239 milioni. Raia huyo wa Marekani anatengeneza fedha kutokana na kazi yake ya uigizaji, uongozaji, utayarishaji na uandishi.

Ameigiza filamu nyingi ikiwemo The Perfect Storm (2000), The Good Man (2006), Tommorowland (2015) na nyingine nyingi. Clooney pia ni mwanaharakati wa masuala ya kibinadamu pamoja na siasa.

Dwayne Johnson maarufu kama “The Rock” ameshuka nafasi moja na kuwa namba mbili baada ya kuongoza orodha hiyo mwaka jana. The Rock anaingiza kiasi cha dola za Kimarekani 119 milioni kwa kazi yake ya uigizaji na matangazo.

The Rock amehusika katika filamu kadhaa ambazo mpaka sasa zinafanya vyema sokoni na hivyo kumfanya avute mkwanja wa maana. Filamu zinazofanya vizuri kwa sasa ni pamoja na Jumanji: Welcome to the jungle, Baywatch na Fast and Furious.

Robert Downey Jr.

Anayefuata katika orodha hiyo ni Robert Downey JR. Downey Jr alilipwa kiasi cha dola 79 milioni ambazo zinatokana malipo ya kuigiza.

Downey Jr ni muigizaji wa Marekani ambaye ana utajiri wa dola 260 milioni unaotokana na kazi mbalimbali anazofanya. Jarida la Forbes linamtaja kama muigizaji mwenye mafanikio zaidi. Hata mshahara anaolipwa katika kazi ya uigizaji pekee inamweka nyuma ya The Rock pamoja na George Clooney. Alipata umaarufu katika sinema zinazofanya vizuri sokoni ikiwemo The Avengers, Iron Man 3, Danger Zone na nyingine nyingi.

Chris Hemsworth ni mzaliwa wa nchini Australia. Amepata umaarufu mkubwa baada ya kujiunga na kampuni ya kupika filamu ya Marvel na kushiriki sinema za kibabe (Action movies) zinazotengenezwa na kampuni hiyo.

Hata hivyo Hemsworth anashika nafasi ya nne katika orodha hii kwa kuweka kibindoni kiasi cha dola 64.5 milioni kama mshahara katika kazi yake ya kuigiza. Alifanya vizuri katika filamu za Thor: The Dark Word, In the Heart of the Sea na Avengers: Infinity War.

Jack Chan ni mwigizaji kutoka Hong Kong anayetamba katika sinema za ndondi, vichekesho na nyinginezo. Pi a ni mwandishi na mwongozaji wa filamu lukuki.

Sio kazi rahisi kumwajiri Jack Chan kucheza sinema yako. Itakulazimu kutumia kiasi cha dola milionio 45.5 ili mcheza kung-fu huyu afanye kazi nawe.

Alitamba na Drunken Master iliyotoka mwishoni mwa miaka ya 1970 kabla ya kufanya vizuri na Te Forbidden Kingdom kisha akaonekana katika Police Story, The Foreigner na nyingine nyingi.

Mmarekani Will Smith amejijengea jina katika ulimwengu wa sinema. Amefanya vizuri katika filamu kadha na kufanya waongozaji wengi kufanya naye kazi. Hivi sasa Will Smith anajiandaa kuwaletea mashabiki wake filamu mbili, Disney’s The Genie na Spies in Disguise.

Smith ni baba wa waigizaji chipukizi Jaden na Willow Smith ambao wanajaribu kufuata nyayo za baba yao. Hata hivyo itakulazimu kuandaa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 42 kama mshahara wake.

Akshay Kumar na Scarlett Johansson

Nafasi hii inashikwa na gwiji wa sinema za kibabe Bollywood (India) Akshay Kumar pamoja na mwanadada kutoka Marekani Scarlett Johansson. Ili uweze kufanya kazi na mastaa hawa wa filamu ni lazima uhakikishe wanaweka kibindoni kiasi cha dola 40.5 milioni kwa kila mmoja.

Mwanadada Scarlett mwenye asili ya Kiyahudi ana utajiri unaotokana na uigizaji, matangazo ya vipodozi na nguo lakini huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uigizaji katika kampuni ya Marvels. Anashika namba moja katika orodha ya waigizaji wanaolipwa mkwanja mrefu kwa upande wa akina dada.

Akshay Kumar ameng’ara zaidi kwa upande wa sinema za kibabe kutoka India. Yeye pia anaingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na matangazo nay a mavazi. Hata hivyo kiasi hicho cha fedha huchangiwa na kazi ya uigizaji kwa kiasi kikubwa. Akshaya anatamba filamu ya Gold ambayo ilitoka mapema mwaka huu,Jaanwar (1999), Andaaz (2003), Boss (2013) na nyingine nyingi.

Adam Sandler. Huyu muigizaji, mwandishi, mchekeshaji na mwongozaji wa filamu kutoka Marekani. Alipata umaarufu zaidi miaka ya 1990 katika filamu ya Billy Madison (1995) na nyingine zilizofuata na kupata mafanikio makubwa katika soko la Hollywood. Kwa sasa anafanya vizuri katika filamu ya The Ridiculous na Hotel Transylvania 3: Sunner Vacation (2018).

Jarida la Forbes linamweka Sandler nafasi ya 8 kwa waigizaji wanaolipwa pesa ndefu katika uigizaji, analipwa dola 39.5 milioni.

Chris Evans

Kampuni ya Marvels inaonekana kushikilia soko la filamu kwani waigizaji wake wanaonekana kutawala orodha hii. Muigizaji mwigine kutoka Marvels, Chris Evans anatajwa katika orodha ya tisa ya waigizaji wanaolipwa kiasi kikubwa cha fedha kama tozo ya kazi yake na jarida la Forbes.

Mkali huyu wa filamu ya Captain America anahitaji kiasi cha dola 34 milioni tu ili aweze kufanya kazi na wewe. Alifanya vyema katika filamu ya Avengers: Infinity War pia alikuwepo katika filamu ya Fantastic Four.

Salman Khan

Huyu staa mwingine kutoka soko la Bollywood baada ya Akshay Kumar kutokea katika orodha ya waigizaji wanaolipwa fedha ndefu. Mzaliwa huyu wa Indore, India alianza kuigiza rasmi mwaka 1989 na kung’ara na filamu kibao mpaka leo.

Hutoza dola 33.5 milioni ili kucheza filamu. Salman Khan muigizaji pia ni mtunzi na mwimbaji wa nyimbo. Anatamba na filamu za hivi karibuni kama Sultan (2016), Tiger Zinda Hai (2017) na Race 3 (2018).