Haya ndiyo maisha ya Havintishi wa Morogoro aliyechangiwa na JPM na kupata Sh1.2 milioni

KUTANA NA MAMA HAVINITISHI, MFANYABIASHARA ALIYELIA KERO MBELE YA JPM

Muktasari:

Ni biashara ndogo, lakini inamuweka mjini Morogoro katika chumba kimoja akibanana na watoto wake wanne na wajukuu wawili.

Morogoro. Alipokuwa amekaa kusikiliza hotuba ya Rais John Magufuli, pengine alikuwa akitaka hotuba iishe haraka ili akaendelee na biashara yake ya kuuza ndizi.

Ni biashara ndogo, lakini inamuweka mjini Morogoro katika chumba kimoja akibanana na watoto wake wanne na wajukuu wawili.

Ni bahati nzuri kwamba katika watoto wake hao, wavulana ni watatu na kila mmoja anajitafutia riziki yake mwenyewe, ingawa jioni wote hukutana hapo kwa malazi katika chumba hicho.

Biashara hiyo ya ndizi mbivu imemsaidia pia kumsomesha mtoto wake pekee wa kike ambaye yupo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Pengine shida na matatizo hayo ndivyo vilivyompa ujasiri mfanyabiashara huyo wa mjini Morogoro Havintishi Mussa (48), kuwasilisha kero kwa Rais John Magufuli katika mkutano wa hadhara Alhamisi na kumuwezesha kuibuka na kitita cha Sh 1.25 milioni.

Ni kama mchezo wa bahati nasibu, alikwenda mkutanoni akiwa hana kitu, lakini akarudi nyumbani na kiasi hicho cha fedha na tayari ameanza kutatua matatizo kadhaa.

Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwake mjini hapa, Havintishi alisema mara baada ya kutoka kwenye mkutano ambako alichangiwa fedha hizo, alisaidiwa na polisi kwenda benki ya CRDB kufungua akaunti.

Pia alibakiza kiasi kingine ambacho alikitumia kulipia chumba kipya chenye hadhi kiasi kuliko cha awali, na jana alichukua kiasi kingine akamtumia fedha za matumizi mtoto wake anayesoma Udom.

Halafu kiasi kingine amekitumia kununua mzigo mkubwa kiasi wa ndizi ili kuendeleza biashara yake.

“Fedha nilizopata zimenisaidia kulipia ada ya mtoto wangu pamoja na kulipia kodi ya chumba,” alisema Havintishi ambaye kuanzia juzi jioni anaishi kwenye chumba kipya, nyumba ya nne hivi kutoka alipokuwa akiishi awali katika Mtaa Mfupi, Barabara ya Boma mkabala na msikiti mkubwa wa mjini Morogoro.

“Nashukuru mara baada ya kupata fedha zile polisi waliniwekea ulinzi ili nisisumbuliwe na walinipeleka moja kwa moja CRDB kwa ajili ya kufungua akaunti.”

Mwanamama huyo alisema kero aliyoiwasilisha mbele ya Rais ni ya muda mrefu na kwa kuwa yeye aliteuliwa kuwa kiongozi wao, alipopata fursa hiyo alipata ujasiri na kuzungumza.

“Nampongeza Rais Magufuli kwa namna anavyowatetea wanyonge na namuomba aendelee na juhudi zake za kuwasaidia kina mama na watoto katika nyanja mbalimbali,” alisema.

Ujasiri

Havintishi, ambaye ni kiongozi wa wafanyabiashara ndogondogo katika stendi ya mabasi madogo mjini hapa, alikuwa miongoni mwa mamia ya wananchi waliojitokeza kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha sigara cha Phillip Moris kilichopo Kingolwira ambako Rais Magufuli alikuwa mgeni rasmi.

Mfanyabiashara huyo alisikiliza kwa makini hotuba ya Rais na kama wanawake wengine alikuwa akishangilia kwa vigelegele.

Rais Magufuli alipotoa fursa kwa mtu mwenye kero, Havintishi ambaye alikuwa mbali na jukwaa la wageni, aliinuka na kunyosha mkono kama walivyofanya wengine na Rais alimchagua yeye ajieleze.

Alipojizoazoa alisema, “Manispaa wanachofanya wao ni kuchukua bidhaa zetu na kututoza faini kubwa na unaposhindwa kulipa bidhaa zinapotelea hukohuko, imefikia mfanyabiashara anashindwa kuendelea na biashara kutokana na kukamatwa mara kwa mara na mgambo wa manispaa.”

Alisema kuwa tatizo lililopo ni kutokuwapo kwa maelekezo yoyote kutoka kwa uongozi wa manispaa na kwamba wao kama wafanyabiashara wanatambua kuwa usafi ni jukumu lao hivyo pindi wanapomaliza kuuza bidhaa zao hufagia na kuuacha mji katika hali salama na wanatambua umuhimu wa abiria na magari yanayoingia katika stendi hiyo.

Baada ya mama huyo kujieleza Rais Magufuli alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula kujibu. Alisema tayari wafanyabiashara wamepangiwa maeneo ya kufanya biashara yaliyopangiliwa na kwamba malalamiko yanayotolewa na wafanyabishara si ya kweli.

Mgalula alitaja maeneo waliyopangiwa wafanyabishara hao kuwa ni Gulio la Kikundi, Sabasaba, Nanenanena Mazimbu na kwamba yanaendelea kufanyiwa ukarabati.

Hata hivyo, Rais Magufuli aliutaka uongozi wa manispaa hiyo kuacha kuwabughudhi na kuagiza waendelee na shughuli zao za biashara.

Rais Magufuli alimchangia mama huyo Sh100,000 na kiasi kingine kufikia Sh1.25 milioni kilichangwa na viongozi, wabunge na wageni waliohudhuria hafla hiyo.