VIDEO: He! Kumbe Bashiru Ally ‘shabiki’ wa Yanga

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa gazeti la Mwananchi, ofisini kwake jijini Dodoma jana. Bashiru amesema kuwa mara moja moja huwa anafurahia timu ya mpira wa miguu ya Yanga kuliko Simba ila amekataa kusema yeye ni shabiki wa timu gani. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Asema anaipenda zaidi Yanga kuliko Simba, ila anaogopa kujiachia wazi atawagawa wanachama wa CCM

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema kuwa mara moja moja huwa anaifurahia  timu ya mpira wa miguu ya Yanga kuliko Simba.

 

Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Dodoma Bashiru, amesema anaogopa kusema moja kwa moja kuwa ni shabiki wa timu gani kwa kuhofia kukigawa chama chake.

 

“Mimi ni shabiki wa mpira, timu gani sisemi kwa sababu nisije nikakigawa chama. Wakati natafuta wanachama halafu ikawa kero lakini mara moja moja sana nafurahia Yanga kulikoni Simba,” amesema.

 

Kwa upande wa sekta ya michezo, Bashiru amesema sekta ya michezo ni sehemu ya utamaduni na ndio inayojenga hali ya kujiamini kwa wananchi.

 

“Na mwalimu (Julius Nyerere) alishawahi kusema utamaduni ni roho ya Taifa. Zipo sekta mbalimbali za sanaa, michezo, riwaya, ngoma na kadhalika. Mimi ningependa kuona sekta zote zinaimarika hasa kwa lengo la kuwajengea ari ya kujiamini Watanzania,”amesema.

 

Amesema jukumu kubwa la wanamichezo ni kutangaza uzuri wa nchi, historia, mapambano ya uhuru, mshikamano, umoja, mahusiano mema, utulivu na raha ya Watanzania.

 

“Mimi mwenyewe ni mshairi, nikipata nafasi naimba, natunga kidogo mashairi na mengine nimeyachapisha. Mashairi yangu ukiyasoma yanafikirisha kidogo. Ninapenda kusoma mashairi ya watu wengine akiwemo baba wa Taifa,”amesema.

 

Hata hivyo, Dk Bashiru amesema katika michezo alikuwa akicheza mpira lakini hivi sasa hawezi kucheza kwa sababu ya kukosa muda na maumivu ya miguu pindi anapotembea sana.