Sunday, November 19, 2017

Heche kujisalimisha polisi

 

By Amina Juma, Mwananchi asangawe@mwananchi.co.tz

Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema kesho ataripoti polisi mkoani Morogoro kuitikia wito wa jeshi hilo.

Heche alisema jana kuwa ana taarifa kwamba anatafutwa na jeshi hilo na anatakiwa kwenda kuhojiwa mkoani Morogoro.

Heche, pia alidai kuwa polisi walikuwa wamkamate, hata hivyo hilo halikufanyika.

Mbunge huyo alisema hajui kosa alilotenda, isipokuwa anatakiwa kuhojiwa kwa kauli alizotoa alipomsindikiza mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kutoka gerezani.

Akizungumza na gazeti hili, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema kwamba mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara wilayani Kilombero Aprili 8, 2017.

Alisema kwamba wanamtafuta kwa tuhuna za kutotii amri za viongozi na kufanya mkutano kisha kutoa lugha za matusi zilizotaka kusababisha vurugu.

Alisema tangu siku ya tukio, jeshi hilo limekuwa likimtafuta mbunge huyo bila mafanikio ndipo lilipoamua kulishirikisha Bunge.

Polisi iliandika barua kwa Spika wa Bunge kumtaarifu kuwa mbunge huyo anatafutwa kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili mkoani Morogoro.

“Barua ni mambo ya siri kati ya jeshi na Bunge, tunachotaka sisi ni kumuona Heche hapa na asitake tutumie nguvu,” alisema Kamanda Matei.

-->