Wednesday, January 17, 2018

Hesabu zilivyo ngumu kwa vyama vya siasa kuelekea uchaguzi 2020

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulimalizika miaka miwili ni miezi mkadhaa iliyopita na joto la kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 limeendelea kupanda kupitia matukio mbalimbali ya kisiasa, ingawa bado ni kwa kasi ndogo kuliko ilivyotarajiwa.

Katika uchaguzi huo uliokuwa wa vuta nikuvute, vyama vinane vilisimamisha wagombea urais, kati ya 22 vilivyoshiriki uchaguzi huo ambao Dk John Magufuli wa CCM aliibuka kidedea akipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47, akifuatiwa na Edward Lowassa wa Chadema aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97. Wengine walipata chini ya asilimia 1.

Katika majimbo 264 ya ubunge, CCM ndiyo iliibuka na mafanikio makubwa ikijipatia 195, Chadema (35), CUF (32), ACT-Wazalendo (1), NCCR Mageuzi(1).

Kwa hesabu hizo za matokeo ya nyuma, ukiongeza na chaguzi ndogo zinazoendelea na hali ya kisiasa ilivyo sasa nchini ambapo wanasiasa hawaruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara wala maandamano, unaweza kujiuliza maswali mengi bila majibu kuhusu mustakabali wa vyama.

Wakati hali ikiwa hivyo, kwa upande mwingine harakati zinaendelea kuelekea mwaka 2020. Mathalan, CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole inatamba itashinda kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura zote za urais. Inasema imeongeza idadi ya madiwani na wabunge wanaohamia kwake na kwamba hata wanachama wameongezeka kwa milioni mbili na zaidi.

Hali hiyo pia inawashtua wachambuzi wa duru za kisiasa, wanasema si sahihi kupima ushindani wa vyama vya siasa kuelekea uchaguzi huo kutokana na mazingira ya hali ya kisiasa kwa sasa.

Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anazungumzia hali hiyo akisema,

“Hakuna uhuru wa kukosoa, siyo vyama vya upinzani tu hata baadhi ya watumishi na viongozi wa umma wanaogopa kutoa taarifa za kuikosoa Serikali.”

Anaongeza, “Taasisi za utafiti, taasisi za kiraia, zinazotetea haki na hata baadhi ya wasomi pia wanaogopa kuikosoa Serikali, kinachokubalika ni kuipongeza tu, katika mazingira hayo kunakuwa hakuna usawa katika ushindani,” anasema Profesa Bakari.

Msomi huyo anasema pamoja na mazingira hayo, bado ni mapema sana kutabiri mauti ya vyama vya upinzani katika uchaguzi ujao kutokana na tabia za wapiga kura kwa akuwa matukio yatakayotokea katikati ya mwaka 2018 na 2020 ndiyo yatatoa ishara za kuamua hatma ya ushindani katika uchaguzi huo.

“Inawezekana kabisa hata hili tatizo la kuzuiwa kufanya siasa likasaidia kuongeza nguvu, siku watakaporuhusu waanze kukaa majukwaani kwa uhuru, wananchi watakuwa na hamasa kubwa pengine kujua nini watakisema,” anasema Profesa huyo.

Nguvu vijijini

Pamoja na mtazamo huo wa Profesa wa Siasa, mwelekeo huo unatoa taswira ya kuwapo mkakati wa kuimarisha vyama vijijini. Polepole kupitia ukurasa wake wa Twitter, anasema CCM imefanikiwa kukusanya idadi ya wanachama wapya milioni mbili tangu 2015.

Polepole anasema CCM itapewa kibali na wananchi katika uchaguzi ujao baada ya Serikali kujikita kutazama masuala matatu – uchumi wa nchi, ustadi wa watu (Watanzania) pamoja na ulinzi, usalama na uongozi bora.

Mbali na uchaguzi wa Rais, katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, CCM ilipata ushindi vijiji/mitaa 9,406 huku vijiji/mitaa 3,211 ikibaki kwa vyama vya upinzani. Mbali na wenyeviti hao wanaoongeza nguvu vijijini, pia, CCM imekuwa ikijivunia mizizi mirefu kupitia viongozi wake wa mashina, matawi na vitongoji nchi nzima.

Na huko vijijini ndiko Polepole anasema CCM imeongeza idadi ya wanachama wapya milioni mbili hivyo kufikia wanachama milioni kumi kuelekea uchaguzi huo, lakini hukohuko pia ndiko wapinzani

wanashindwa kwenda kufanya siasa za kuongeza wanachama. Katika uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani ambao wapinzani wanaendelea kususia, CCM inaongeza majimbo na kata zaidi.

Wakati CCM ikiwa hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema hata wao wanapambana kulingana na mazingira yalivyo. Anasema shughuli za ujenzi wa chama zinaendelea na kwa makadirio wanao wanachama hai milioni nne na wanaendelea kukusanya taarifa za wanachama wapya.

“Kwa ngazi ya chini, tunajivunia kufikia Watanzania katika asilimia 68 ya vitongoji (misingi) vyote nchini. Lakini, viongozi wetu katika maeneo hayo wanabambikiwa kesi na kukamatwa na polisi,” anasema.

Julai 8, mwaka jana viongozi na wanachama 51 wa Chadema walikamatwa na polisi wakiwa kwenye kikao cha ndani wilayani Chato na waliendelea kushikiliwa na polisi kwa mahojiano kwa zaidi ya wiki kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Miongoni mwa waliotiwa mbaroni ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Fabian Mahenge na Katibu wake, Sudi Kanganyala. Mwenyekiti wa Serikali kijiji cha Mkuyuni, Anaclet Twegosora, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho Kata ya Chato.

Kwa ngazi za juu, Dk Mashinji anasema ushiriki wa siasa kwa njia ya matukio ambayo ilikuwa umezoeleka kwa wanachama wao umewekewa vikwazo, hali iliyochagiza chama kuonekana kama kimepooza.

“Matukio ilikuwa ni sehemu tu ya shughuli za chama ila ilionekana kama njia pekee, tunategemea sana local areas (maeneo ya vjijini) kwa sasa, ili kuimarisha misingi ya chama,” anasema Dk Mashinji.

Vyama vichanga

Wakati miamba, CCM na Chadema, wakitamba vijijini, vyama visivyokuwa na uwakilishi vimedaiwa kupoteza matumaini siku hadi siku kutokana na mazingira ya kisiasa kuelekea 2020.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama visivyokuwa na uwakilishi bungeni, Renatus Muhabi anasema hali ni mbaya kwa vyama hivyo, hatua inayokatisha tamaa ya kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Muhabi anasema kutokana na kufifia kwa matumaini, viongozi wa vyama hivyo wamepanga kukutana kwa ajili ya vikao vitakavyotoa hatima yao. Vyama hivyo ni Chama cha Wakulima (AFP), DP, Demokrasia Makini, UPDP, Chama Cha Kijamii (CCK), ADC, TLP, UMD, NRA, Ada-Tadea na Sauti ya Umma (SAU).

“Kwa sababu vyama vyetu vinakuwa kama wasindikizaji tu, kwa mfano uchaguzi wa kata 43 na huu wa majimbo uliomalizika, hakuna ushindani wowote ulioonekana, wanaopewa ruzuku walisusia, hatuogopi kushiriki lakini tatizo ni mazingira yalivyojengwa kisiasa na kimfumo,” anasema Muhabi.

Muhabi anataja matatizo matatu ambayo yataendelea kuwa kikwazo kwa vyama vya upinzani kuwa ni kukosekana Tume huru ya Uchaguzi kupitia Katiba mpya itakayobadili mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Mwenyekiti wa NEC amepewa mamlaka kisheria ya kuteua mtumishi yoyote kutoka taasisi za Serikali ili amsaidie kazi, sasa unateua mtumishi asimamie uchaguzi ambao Rais aliyemwajiri ndiye mgombea, kwa mazingira hayo kwa nini CCM isishinde kata 42 kati ya 43?

Anaongeza, Mkurugenzi wa halmashauri ambaye ni msimamizi wa uchaguzi atafanyaje katika uchaguzi unaohusisha chama chake?” Muhabi anasema mfumo wa ruzuku wa Serikali hautoi nafasi ya usawa katika ushindani wakati wa uchaguzi kutokana na ubaguzi wa vyama na kuvifanya baadhi visiweze kufanya vizuri.

Anasema vyama vyenye wagombea vinatakiwa kupewa ruzuku kwa usawa ili kufanya kampeni za ushindani.

“Mwenzio anatumia helkopta, wewe unatumia genereta ya mafuta ya lita mbili, hata kama una sera nzuri utafika wapi kuzifikisha kwa wananchi?” anahoji Muhabi.

Katibu huyo wa CCK anatupia lawama Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, jinsi ambavyo imeshindwa kusimamia, kuvilea vyama katika usawa bila upendeleo.

Anasema Msajili anatakiwa kutetea sheria ya Vyama vya Siasa inayotoa haki ya kushiriki mikutano ya kujenga vyama.

CCM na nguvu ya rais

CCM ikiwa chini ya mwenyekiti ambaye pia ni Rais imeendelea kucheza vizuri karata yake na kujiimarisha kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015/20 na fursa za shughuli mbalimbali za kiserikali ambayo vyama vingine havina.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa vyama wa upinzani wamekuwa wakilalamika kwamba hata mikutano ya Serikali imetumika kuwapokea wapinzani wanaohamia CCM na wakati mwingine mikutano ilifanyika Ikulu ilifanya hivyohivyo.

Baadhi ya mifano inayotajwa na wachambuzi wa duru za kisiasa ni pamoja na ushawishi kupitia ziara za Rais Magufuli kwenye majimbo ya wabunge wa upinzani, ikiwamo tukio la Julai 23, mwaka jana huko Kaliua (Magdalena Sakaya-CUF), Tanga mjini (Mussa Mbarouk-CUF) na Buyungu (Bilago Kasuku-Chadema) ambao kwa nyakati tofauti walilazimika kuendesha mikutano ya kuelimisha wapiga kura wao.

Tukio jingine ni kupokea madiwani waliojiuzulu kutoka Chadema kuingia CCM, kupitia tukio la kiserikali la kutunuku Kamisheni kwa maofisa 422 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) jijini Arusha.

Pia, kuna sintofahamu kwa Chadema na wanachama wake kutokana na wanaojivua uongozi na kujiunga CCM, wengi wao wakisema wanamuunga mkono Rais Magufuli, jambo ambalo wangeweza kulifanya wakiwa hukohuko.

Polepole anajibu baadhi ya hoja akisema siasa si kufanya mikutano ya hadhara pekee, badala yake kuna siasa za madaraka na siasa za maendeleo, akifafanua kwamba huu ni wakati wa siasa za maendeleo.

“Siasa za madarakani, tunakaa majukwaani ila upo muda mwafaka, hata Marekani na Uingereza wanafanya hivyo, lakini Rais amesema kila mbunge afanye sias akwenye jimbo lake, Rais wa ni mbunge wa nchi nzima kwa hiyo anayo haki ya kufanya siasa eneo lolote,” anasema Polepole.

Vilevile, Polepole anasema si rahisi kumtofautisha Rais na nafasi zake katika majukumu mengine, hivyo CCM inatekeleza Ilani yake na wakati huohuo Rais ndiye mwenyekiti wa CCM.

-->