Hii ndio siri ya biashara ya dawa za kulevya-1

Muktasari:

Tangu kuanza kwa vita hiyo katikati ya miaka ya 90, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya Tanzania na kwingineko duniani, wamekuwa wepesi katika kubadili mbinu ili kukwepa jicho na mkono wa dola.

Watu walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kama vile cocaine, heroin na bangi wanadai hakuna vita ngumu, hatari na inayohitaji kubadili mbinu kila wakati kama ilivyo vita dhidi ya uuzaji na utumiaji mihadarati.

Tangu kuanza kwa vita hiyo katikati ya miaka ya 90, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya Tanzania na kwingineko duniani, wamekuwa wepesi katika kubadili mbinu ili kukwepa jicho na mkono wa dola.

Katika siku ya kwanza ya mfululizo wa makala za kusisimua zinazofichua jinsi wauzaji na watumiaji wanavyobadili mbinu za kufanya biashara hiyo haramu, tunaanza kwa kukuletea maisha ya msiri wetu na jinsi alivyojikuta akitumika kufanya biashara ya mihadarati. Endelea…

Macho mekundu, sauti nzito yenye kukwaruza, na nguo chafu na kuukuu alizovaa vinatosha kumtambulisha *Mashikolo. Siku nilipoanza uchunguzi kuhusu hali ilivyo baada ya Serikali kuongeza nguvu katika kupambana na dawa za kulevya na usiri uliopo katika biashara hiyo, haikunichukua muda kujua kwamba Mashikolo, kijana mfupi, mweusi, mwenye hasira za ghafla zisizodumu lakini mwenye kumbukumbu na uelewa mkubwa wa mambo, ni mtumiaji wa dawa hizo haramu.

Wakati natafakari mbinu gani nitumie kumuingia na kumgeuza chanzo changu cha habari, sikuwa na chembe ya ufahamu ni siri kubwa kiasi gani kijana huyu amebeba kuhusu biashara ya dawa za kulevya jiji Dar es Salaam.

Lakini baada ya kumshawishi na yeye kukubali kunisaidia katika kazi iliyonichukua takriban miezi mitatu, nilibaini dawa za kulevya bado zinauzwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Tofauti ni kwamba watumiaji na wauzaji wamebadili mbinu.

Mashikolo anakiri kwamba yeye amewahi kutumia cocaine na heroin kabla ya kupata matibabu na kuachana nazo. Sasa anatumia bangi pekee. Mbali na kunionyesha maeneo na watu wanaofanya biashara hizo, ananisaidia pia kufichua usiri mkubwa unaotumika kuendesha biashara hiyo baada ya Serikali kuanza kuvunja mitandao ya wafanyabiashara wakubwa.

Mashikolo alianza kutumia dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka 24 na amewahi kufanya kazi ya kuzisafirisha kutoka Afrika Kusini kwenda Zambia na Tanzania kwa zaidi ya miaka miwili.

Siku ya kwanza kuonana naye eneo la Mnazi Mmoja kilipo kijiwe chao, nilimuogopa kutokana na muonekano wake. Lakini baada ya kujenga mazoea nikagundua si mtu mbaya kama anavyoonekana.

Nilitamani kufa

Siku moja tukiwa katika kijiwe anachofanya kazi kama msimamizi wa wazoataka za barabarani, maofisini na majumbani maeneo ya Mnazi Mmoja, Mashikolo alizungumzia maisha yake kwa hisia kali.

“Dada, watu tumetoka mbali, usituone tuko hivi. Ilifika wakati nikatamani kufa niondoke duniani maana niliona dunia na jamii vimenitenga,” anasema Mashikolo.

“Nilizaliwa kwa bahati mbaya dada yangu. Mama yangu alipata mimba akiwa bado mdogo, tena na mwanaume aliyempa aliukataa ujauzito. “Familia ya mama yangu walishika sana dini, hivyo waliamini msichana kupata mimba kabla hajaolewa ni mkosi kwa familia hivyo ukoo ukamtenga.

“Baada ya kutengwa mama hakuwa na msaada wowote, na mwanaume aliyempa mimba akatoroka. Maisha yakawa magumu kiasi kwamba mama yangu alifariki kutokana na msongo wa mawazo miezi miwili tu baada ya kunizaa.”

Mashikolo anatembea kwa kuchechemea kidogo. Mguu wake wa kushoto umekuwa mfupi kutokana na kuumia ajalini.

Anasema baada ya matanga, ukoo ulikaa na kutaka kumtupa lakini bibi yake mzaa mama akajitolea kumlea.

“Nikiwa na umri wa mwaka mmoja, bibi yangu alitaka kuniua. Siku moja wakati ananiogesha, aliamua kunipigiza chini,” anakumbuka.

“Nilivunjika mguu wa kushoto, mfupa wa nyonga ukaachia na kutokeza nje. Ni kama Mungu tu sikupoteza maisha bali nilibaki kuugulia maumivu. Nimekaa na mfupa wangu nje kwa zaidi ya miaka 20 hakuna mtu aliyenitibu mpaka nilipopata msaada wa kuchukuliwa na kituo cha kulea watoto yatima(alikitaja).

“Kituo hicho kilinipa msaada wa matibabu kwa kunipeleka nchini India ambapo nilifanyiwa upasuaji na nikapona. Lakini kipindi chote kabla ya kuchukuliwa na kituo hiki nimeishi maisha ya shida.Tangu kukua kwangu sikuwahi kutembea nilikuwa ni mtu wa kujivuta.”

Anasema maisha yake ya utotoni hakuwa akipata chakula ipasavyo na ilifika wakati alipokuwa na umri wa miaka mitano, alianza kwenda kwenye nyumba za majirani kuvizia chakula. Wakati akieleza hayo, ghafla anakuja kijana mmoja, anamchukua na kuondoka naye.

Nikabaki nikitafakari historia ya kusikitisha ya Mashikolo. Nikiwa katika kijiwe kile niliendelea kushuhudia watumiaji dawa za kulevya, maarufu kwa jina la ‘mateja’, wakiingia eneo hilo na kutoka.

Walikuwa wakivuta sigara, bangi na kunywa gongo iliyokuwa ikiuzwa na Mashikolo. Ilipofika jioni, niliamua kurudi nyumbani.

Nilikuwa katili

Baada ya kupita siku kadhaa, nilirudi tena kwa Mashikolo. Safari hii nilikaa naye hadi saa 4:00 usiku, nikitaka kujua mengi zaidi kuhusu biashara ya mihadarati na jinsi alivyofanya kazi ya kusafirisha dawa za kulevya.

Anasema biashara inahitaji ujasiri na roho ngumu. “Ilifika wakati nikawa katili. Watu waliniogopa kutokana na mateso niliyoyapitia. Mimi nimewahi kutumia dawa za kulevya, tena ule unga wenyewe sio huu feki wanaotumia sasa,” anasema Mashikolo.

“Nimefanya uhalifu mwingi kama kubeba unga kutoka Afrika Kusini na kupeleka Zambia wakati mwingine Tanzania. Nilifanya hivi si kwa kutaka, bali kutafuta maisha.”

Anasema walikuwa kundi kubwa la vijana wakati wanaondoka kwenda Afrika Kusini, ingawa hakumbuki mwaka lakini anasema wakati huo biashara hiyo ilikuwa imeshika kasi. Anasema walitumia njia za panya. Walipanda maroli hadi Kapirimposhi, Zambia.

“Tukatembea na kuvuka eneo moja ambalo ni jangwa tupu hadi tukafika Afrika Kusini. Lengo lilikuwa ni kwenda kufanya biashara ya dawa za kulevya baada ya kuambiwa huko inalipa,” anasema.

“Pia tulikwenda kufanya ujambazi na uporaji. Tulipofika tukapata dili la kubeba dawa za kulevya kutoka kwa jamaa mmoja Mtanzania (anamtaja jina) tukizitoa Afrika Kusini na kuzileta Zambia na nyingine Tanzania.

“Huyu jamaa kazi yake ilikuwa ni kutafuta makontena (wabeba dawa za kulevya) na kuwatafutia paspoti na vibali vya kwenda nchi mbalimbali.” Anasema mtu huyo alikuwa akiwalipa fedha kulingana na ukubwa wa mzigo na pesa hiyo ilikuwa ikilipwa pale mzigo utakapofika salama.

“Tulikuwa tunabeba unga kwa kuingiziwa sehemu za kutolea haja kubwa kwa wanaume lakini kwa wanawake walikuwa wakijaziwa sehemu za haja ndogo na kubwa na wengine walikuwa wakifanyiwa upasuaji na kuwekewa tumboni,” anasema.

“Tulitumia njia nne kufikisha mzigo unapotakiwa. Huyu jamaa alikuwa anatukatia tiketi ya ndege na kutukabidhi kwa marubani wa ndege na wahudumu waliowasiliana na watu wa uwanjani ambako ndenge ingetua.

“Tunakuwa ni watu wa mwisho kushuka kwenye ndege, abiria wote watashuka na baadaye huja mtu wa kutupokea kama ndugu zake. Huyu anakuwa anajuana na watu wa uwanja wa ndege na wafanyakazi wa ndege tuliyoshuka.”

Mashikolo anasema walikuwa hawakaguliwi uwanja wa ndege na walikuwa wakichukuliwa moja kwa moja hadi katika gari lililoandaliwa na kwenda kuzitoa dawa hizo.

“Mnapotaka kuzitoa kwanza mnapewa chakula cha kutosha halafu mnapewa dawa za kuharisha. Ukijisaidia dawa zote zinatoka na unapewa pesa yako.”

Anasema hawakuwa wakipanda ndege moja wabebaji wote. Tajiri aliwaganywa katika ndege tofauti.

“Wenzetu waliobeba tumboni walisafiri kama wagonjwa mahututi na waliambatana na daktari ambaye muda wote huwaangalia. Wanaposhuka uwanja wa ndege hupelekwa moja kwa moja hadi hospitali iliyoandikwa hata kwenye vibali vyao vya kusafiri,” anasema.

“Wanapofika huingizwa kwenye chumba cha wagonjwa maalumu ambako hufanyiwa upasuaji mwingine kutoa dawa hizo. Kumbuka Daktari na wote wanaohusika katika mpango nao huambulia si chini ya Sh5 milioni kila mmoja.”

Anasema yeye alikuwa anatumia haja kubwa.

“Tulikuwa tunaingiziwa dawa kwa njia ya vidole na zile kete zilikuwa zinapakwa mafuta ya kulainisha na sehemu ya haja pia inapakwa hivyo zinakuwa zinateleza wakati wa kuingizwa.”

Anasema ili kubeba kwa njia hiyo, ni lazima upigwe bomba kwanza (ufanye mapenzi kinyume na maumbile)kwa kuwa waliambiwa kuwa hiyo husaidia kurahisisha wakati wa kuziingiza na kuwa na nafasi kubwa.

“Nilikuwa najaziwa mpaka zinagusa eneo la kitovu,” anasema.

Mashikolo anadai kwa kutumia usafiri wa basi, wabebaji walishonea nguo iliyojazwa dawa za kulevya na kuivaa na wanawake walishonewa kwenye nguo zao za ndani au begi la nguo.

Mashikolo anasema kwa usafiri wa meli, mzigo ulijazwa kwenye meli za mizigo na kushushwa bandarini au kufaulishwa kwenye boti za wavuvi . Njia nyingine ilikuwa ni njia za panya, anasema.

Itaendelea kesho