Hivi hapa vikwazo vya kielimu kwa wasichana

Muktasari:

Takwimu za elimu za Serikali zinaonyesha kuwapo kwa uwiano wa 1:1, baina ya watoto wa kike na watoto wa kiume, wanapoandikishwa kusoma darasa la kwanza.

Ingawa elimu ni haki ya kila mwananchi, ripoti mbalimbali zinaonyesha kwamba watoto wa kike wanakumbana na changamoto nyingi, ambazo kwa kiasi kikubwa zinasababisha wabaki nyuma kielimu tofauti na hali ilivyo kwa watoto wa kiume.

Takwimu za elimu za Serikali zinaonyesha kuwapo kwa uwiano wa 1:1, baina ya watoto wa kike na watoto wa kiume, wanapoandikishwa kusoma darasa la kwanza.

Hata hivyo, ni asilimia tano hadi sita pekee ya watoto wa kike ndio wanaofanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari ukilinganisha na asilimia 12 hadi 13 ya wavulana.

Hali hii kimsingi, inaathiri hata idadi ya wasichana wanaofanikiwa kufika ngazi za juu za elimu ikiwemo ngazi ya chuo kikuu.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya Shirika la Haki za Binaadamu ( Human Rights Watch) ya mwaka 2017, kuhusiana na vikwazo vya elimu ya sekondari nchini, miundombinu duni ya shule, kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na mimba za utotoni, ni baadhi ya vikwazo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinarudisha nyuma elimu ya mtoto wa kike. Tukizungumzia miundombinu ya shule ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, umeme, matundu ya vyoo pamoja na madarasa.

Kwa mujibu wa takwimu za elimu za taifa (BEST) za mwaka 2016, ni asilimia 43.6 tu ya shule za msingi na asilimia 54.4 ya shule za sekondari nchini ndizo zenye huduma ya maji.

Ukosefu wa maji safi pamoja na vyoo salama shuleni, imekuwa ni changamoto kubwa kwa watoto wa kike kwani hupata wakati mgumu kujisitiri hasa wakiwa katika kipindi cha hedhi.

Wakati mwingine huwalazimu kukosa masomo katika kipindi chote wanapokuwa kwenye mzunguko wa wa siku zao. Mazingira duni ya shule kama haya yanachangia wasichana kutofanya vizuri kwenye masomo yao na wakati mwingine kuacha shule.

Shule za bweni zinatajwa kuwa ni suluhisho hasa kwa wanafunzi wa kike wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.

Hata hivyo, shule za bweni ni chache ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi, hali inayowalazimu baadhi ya wazazi kuwapangishia watoto wao nyumba mitaani, ili waweze kuwa karibu na shule.

Mazingira haya nayo yamekuwa siyo salama kwa wasichana, kwani wengi wamejikuta wakikatisha masomo kutokana na changamoto lukuki zinazowazonga za kiuchumi na kijamii, mwishowe wapo wanaoishia kupata ujauzito.

Aidha, taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba wanafunzi wengi wa kike wanaotembea umbali mrefu kwenda shuleni wanakuwa kwenye hatari ya kukutana na vishawishi kutoka kwenye jamii kuliko wale walioko kwenye shule za bweni.

Kwa mfano, taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba katika maeneo mengi ya miji, baadhi ya vijana wanaoendesha pikipiki wamekuwa wakiwarubuni wasichana wa shule na kuwapa ujauzito kwa ushawishi wa kuwahakikishia lifti ya kwenda na kurudi shuleni.

Hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na mwamko mdogo na uelewa hafifu wa umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike kwa baadhi jamii, hali iliyosababisha watoto wa kike kuendelea kubaki nyuma.

Kwa mfano, baadhi ya jamii zinaona kumsomesha mtoto wa kike ni hasara, kwani anaweza kupata ujauzito na hivyo fedha kupotea bure. Katika jamii hizi, elimu kwa mtoto wa kike haionekani kuwa na umuhimu wowote.

Zipo baadhi ya jamii huwakatisha masomo watoto wao wa kike na kuwaoza ili kujipatia mali kwa njia ya mahari. Vilevile, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na ugumu wa maisha, mtoto wa kike amekuwa akitwishwa mzigo mkubwa wa kulea familia.

Ni kawaida kumkuta mtoto wa kike kwenye baadhi ya jamii ameachiwa majukumu yote ya nyumbani kama vile kulea watoto na wakati mwingine kulazimika kufanya kazi au biashara ndogondogo, ili kupata fedha, chakula na mahitaji mengineyo.

Kwa kiasi kikubwa, mtoto wa kike anakutana na vikwazo vingi vinavyosababisha abaki nyuma kielimu ambayo ni muhimu katika kumkomboa kiuchumi na kijamii.

Kuna usemi maarufu unaosema: “Ukimuelimisha mwanamke, umeielimisha jamii”; Mtoto wa kike ana mchango mkubwa katika jamii, kwani ni mama na pia ni mlezi wa familia.

Utafiti wa taasisi mbalimbali umethibitisha kwamba mtoto wa kike akipata elimu, ana uwezo mkubwa wa kuitunza jamii yake vizuri, kiafya na hata kijamii.

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba mtoto wa kiume hakutani na changamoto; ila kutokana na sababu za kimaumbile, mazingira, mila na desturi, changamoto hizi zinaathiri zaidi maelfu ya watoto wa kike kuliko wa kiume.

Hivyo, ni muhimu kwa wadau wote wa elimu na jamii nzima kwa jumla kusimama kidete kumnusuru mtoto wa kike kwa kuondoa vikwazo vyote, ili aweze kupata elimu kwa maendeleo yake na taifa kwa jumla.

Rose Kalage ni Ofisa programu wa idara ya utafiti, ubunifu na uchambuzi wa sera- HakiElimu. [email protected]