Hizi ndizo ajenda za kampeni Mhandu

Muktasari:

  • Viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa waliofika Mhandu kuwanadi wagombea wao, akiwamo kiongozi wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe nao walibeba ajenda hizo kushawishi kura kwa wagombea wa vyama vyao.

 Ajenda za ubovu wa barabara, kutopatikana kwa majisafi na salama pamoja suala la afya ndiyo imeonekana kutawala kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Mhandu jijini Mwanza.

Viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa waliofika Mhandu kuwanadi wagombea wao, akiwamo kiongozi wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe nao walibeba ajenda hizo kushawishi kura kwa wagombea wa vyama vyao.

“Mkimchagua mgombea wa ACT-wazalendo, Emily Balahula kuwa diwani wenu, ataishawishi Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji kutenga bajeti kwa ajili ya kuleta maendeleo katika sekta ya maji, afya na miundombinu ya barabara ambayo ndiyo tatizo kuu la wakazi wa Mhandu, bila kusahau ajira kwa vijana,” alisema Zitto.

Ahadi ya kushughulikia kero hizo pia ilitolewa na Mbowe, Novemba 19 alipohutubia mkutano wa kampeni kumnadi mgombea Chadema, Godfrey Missana.

Hata viongozi wa CCM nao hawajabaki nyuma kuhusu ahadi ya kushughulikia kero hizo baada ya Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Raymond Mwangwala kuwaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua mgombea wa, Constatine Sima ili akaungane na madiwani wenzake kutatua kero zinazowakabili.