Hofu yatanda Ikwiriri kutokana na mabomu

Muktasari:

Pamoja na mabomu hayo kusikika na baadhi ya watu kujeruhiwa juzi, wananchi wamekuwa na woga wa kuzungumzia vitendo vinavyoendelea wilayani hapo kutokana na kuhofia maisha yao.

Rufiji. Hali ya wasiwasi imezidi kutanda katika mji wa Ikwiriri mkoani Pwani baada ya mabomu kusikika yakirindima usiku wa kuamkia jana.

Pamoja na mabomu hayo kusikika na baadhi ya watu kujeruhiwa juzi, wananchi wamekuwa na woga wa kuzungumzia vitendo vinavyoendelea wilayani hapo kutokana na kuhofia maisha yao.

Mabomu hayo yalisikika maeneo ya Kaunda, Mwembe Mohoro, Stendi pamoja na eneo la Mtiga lililopo katika Kata ya Umwe.

Mshtuko wa mabomu hayo ulisababisha wanawake wanne kulazwa kituo cha afya Ikwiriri wilayani Rufiji baada ya kuzimia.

Kaimu mganga mkuu wa kituo hicho, Dk Hawa Lupenza alisema mmoja kati ya wanawake hao alikuwa mjamzito.

Aliwataja wanawake hao kuwa ni Aisha Mohammed, Theresia Cornel, Zuwena Bugala na Anavick Yohana ambaye ni mjamzito.

Alisema wanawake hao walifikishwa kituoni hapo kutokana na mshtuko wa mabomu ya machozi yaliyopigwa na askari polisi waliokuwa doria katika mji huo.

“Tulipokea wanawake wanne waliokuwa wamezimia kutokana ni milio ya mabomu ya machozi yaliyokuwa yamepigwa na askari polisi katika maeneo mbalimbali hapa Ikwiriri,” alisema.

Alisema baada ya kuwafanyia uchunguzi walibaini wanawake hao walikuwa wamezimia kutokana milio hiyo ya mabomu hivyo kuanza kuwatibu.

Lupenza alisema kwamba wote waliruhusiwa jana baada ya afya zao kuimarika.

Mmoja wa madiwani waliopo Tarafa ya Ikwiriri, ambaye aliongea na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, alisema mabomu hayo yalipigwa na polisi kuanzia saa 12:30 jioni juzi.

Alisema hakuna mtu anayefahamu sababu za askari kupiga mabomu hayo na akawataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano kwa polisi.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga kuzungumzia tukio hilo, hazikuzaa matunda.