Hoja ya Nape yawakutanisha mawaziri watano

Hoja ya Nape yawakutanisha mawaziri watano

Muktasari:

Kufuatia hoja hiyo, mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi alionekana akiteta na mawaziri kadhaa ndani ya Bunge.

Dodoma. Baada ya juzi mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kudai waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amevunja sheria na kanuni zinazosimamia wanyamapori kwa kufuta leseni za uwindaji katika vitalu, jana aliendelea na msimamo wake.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii juzi, Nape alisema barua na matamko mbalimbali ya wizara hiyo yameikosesha Serikali mapato kwa kuwa zaidi ya vitalu 18 vimerudishwa na waliokuwa wakimiliki na kufanya jumla ya vitalu vilivyo wazi kuwa 81 kati ya vitalu 159.

“Uchambuzi unaonyesha tamko la Oktoba 23, 2017 na barua ya Desemba 29, 2017 zimetolewa kinyume cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake ambazo zimeweka bayana utaratibu wa kumilikishwa kitalu cha uwindaji na utaratibu wa kufutiwa leseni kwa anayekiuka masharti,” alisema Nape.

Hoja mpya

Jana kwa mara nyingine alilitikisa Bunge kwa kuitaka Serikali kusitisha mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge katika Pori la Akiba la Hifadhi ya Selous na kusababisha mawaziri watano wakutane kwa ‘dharura’ ndani ya Bunge.

Hoja ya Nape kuhusu mradi huo ambao wadau wa mazingira wamewahi kutahadharisha juu ya athari za kimazingira zinazoweka kujitokeza, iliungwa mkono na baadhi ya wabunge akiwemo Zitto Kabwe (Kigoma Mjini ACT-Wazalendo), James Mbatia (Vunjo NCCR-Mageuzi) na Susan Kiwanga (Chadema-Mlimba).

Kufuatia hoja hiyo, mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi alionekana akiteta na mawaziri kadhaa ndani ya Bunge.

Mawaziri hao ni Dk Kigwangalla; wa Madini, Angellah Kairuki; wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; wa Nishati, Dk Medard Kalemani na waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.

Akichangia katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19, Nape alimtaka Dk Kilangi aisaidie Serikali kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopitishwa na Bunge.

“Kwa unyenyekevu sana Serikali naiomba isitishe zoezi hili isubiri tathmini ya kimkakati ya mazingira ikamilike. Mbuga ya Selous inahusisha mikoa mitano; Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Haiwezekani tukapuuza maisha ya watu, wanyama, mimea na viumbe mbalimbali katika mikoa mitano ya nchi,” alisema na kushangiliwa na baadhi ya wabunge.

Selous ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), lakini uamuzi wa Serikali kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 ikitumia zaidi ya Dola2 bilioni (zaidi ya Sh4.5trilioni) katika uwekezaji wake unaelezwa kuwa huenda ukaliondoa pori hilo kwenye orodha hiyo.

“Wakati tunakamilisha taarifa ya kamati Aprili 25, mwaka huu TFS (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ) walitangaza tenda ya kukata miti kwenye Pori la Akiba la Hifadhi la Selous. Tenda hii inahusisha ukataji wa miti zaidi ya qubic meter (mita za ujazo) 3,495, 362,” alisema Nape.

“Ukisikiliza tafsiri ya idadi ya miti itakayokatwa ni sawa na ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam na zaidi na wapo wanaosema ni ukubwa wa Unguja nzima.”

Mbunge huyo alisema Bunge lilitunga sheria namba 20 ya mwaka 2004 ya usimamizi wa sheria, kwamba sehemu ya saba ya sheria hiyo inazungumzia tathmini ya mazingira kimkakati, ikiwemo kufanyika kwa tahmini ya mazingira.

Alisema mpaka jana, tathmini hiyo haijakamilika na bado inaendelea kufanywa, lakini TFS wametangaza tenda ya kukata miti hiyo.

Nape alisema ni vyema tathmini hiyo ikasubiriwa ifanyike, “ikija hata kama tunataka kuendelea na mradi itatueleza wapi tukanyage na wapi tusikanyage, tutaokoa maisha ya watu hawa.”

Akizungumzia suala hilo, Zitto alisema: “Naomba niwe muwazi kabisa, hakuna mtu anayepinga nchi yetu kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme. Tunataka taratibu za kisheria, utunzaji wa mazingira kufuatwa na kuhakikisha nchi haiathiriki kutokana na mradi mmoja ambao tayari una mbadala.”

“Nape kasema hili, ila ukweli ni kuwa ukikata miti ambayo ni sawa na ukubwa wa Dar es Salaam yenye square kilometre (kilomita za mraba) 1,360, miti ile ipo eneo la square kilometre zaidi ya 1,400…, tena eneo ambalo miti hii inakwenda kuondolewa ni eneo ambalo lina unyevuunyevu na wanyama wakitafuta maji huenda hapo.”

Zitto pia aligusia athari za kiuchumi zinazoweza kujitokeza, akitolea mfano mkakati wa Tanzania kwamba unapofika mwaka 2025 kuwe na watalii milioni nane watakaoingiza Dola 16 bilioni za Marekani kwa mwaka. “Watalii hawa hawatakwenda maeneo ya Kaskazini pekee, sasa ukiiondoa Selous yote unafikiaje mikakati hii, tunalinganishaje mikakati na mipango tunayoifanya?” alihoji.

“Tuna mbadala wa kuzalisha umeme, tuna bomba la gesi linalotumika kwa asilimia sita tu. Naomba jambo hili tulitazame kwa umakini maana tunakwenda kupoteza maana ya kukuza utalii katika nchi tusipokuwa makini na namna tunavyoshughulika na Stigler’s Gorge.”

Alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwahi kuwa mwanafunzi na pia alifanya kazi Selous na kumtaka atafakari uondolewaji wa miti hiyo.

“Historia yako (Spika) itakuwa imekufa kabisa,” alisema.

Kwa upande wake, Mbatia alisema, “Kwa miaka minne mfululizo, kuanzia 2012 hadi mpaka 2016 utalii ulikuwa unakua kwa asilimia 13.98, ila 2017 umeshuka mpaka asilimia 3.3 na hii inatokana na kutotekelezwa kwa sheria na matamko ya ajabuajabu, Serikali imewahi kusema mpaka 2020 utalii utakuwa umekua kwa asilimia 30, kulikoni kwa Serikali ya Awamu ya Tano.”

Mbunge huyo alisema katika sekta ya utalii nchini kuna kodi zaidi ya 57 na kubainisha kuwa Dubai wamefuta kodi katika sekta ya utalii na kutoa viza kwa wageni zaidi ya miaka 10 kuwekeza katika utalii, huku Tanzania ikitoza kibali cha utalii kwa wageni kwa Dola 4,000 za Marekani kwa miaka miwili hadi minne.

Alisema ili watalii waweze kuingia nchini ni lazima Serikali iwekeze kwenye miundombinu ya utalii na kutaka utalii kutangazwa na mashirika ya habari ya nje na si Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Naye mbunge wa Bunda Vijijini, Boniphace Getele (CCM), alisema angepinga kama fedha zinazotolewa kutekeleza mradi wa Stigler’s Gorge zitaathiri maeneo mengi kama kilimo, viwanda na sio kwa suala la kukata miti.

Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema Tanzania ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki ina rasilimali nyingi, lakini iko nyuma kwa sababu ya kupanga vitu halafu baada ya muda huondolewa.

Kiwanga alisema kuna asilimia karibu 60 za maji kutoka eneo la Kilombero litachukuliwa katika utekelezaji wa mradi huo, lakini pamoja na kuwa na mpango huo Serikali haizungumzii kuhusu athari zitakazotokana mradi.