Hospitali 10 zapewa mashine za Ultrasound kuboresha huduma

Muktasari:

  • Zimebainika kuwa na sifa za kuzalisha wajawazito wengi na uongozi shirikishi unaotunza mashine

Hospitali 10 za Serikali zilizoonyesha jitihada za kuokoa maisha ya mama na mtoto zimekabidhiwa mashine za Utrasound zenye thamani ya Sh143 milioni.

Hospitali hizo zilizopatiwa mgao wa mashine hizo za kisasa aina ya GE Vscan Access ni Amana, Mwananyamala, Mnazi Mmoja, Buguruni, Kimara, Tandale, Temeke, Sinza, Mbagala Rangi Tatu na Vijibweni.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda aliwapongeza wauguzi na madaktari walioko mstari wa mbele kuokoa maisha ya mama na mtoto.

“Mashine hizo zitasaidia katika utambuzi wa mapema wa matatizo ya uzazi yanayohitaji mjamzito kuwahishwa katika hospitali kubwa kwa msaada zaidi,” alisema Makonda.

Hospitali hizo ni miongoni mwa zenye sifa za kuzalisha wajawazito wengi, utendaji wa pamoja na uongozi shirikishi unaotunza mashine.

Alisema uchaguzi wa vituo hivyo ulizingatia viashiria vya utendaji vilivyowekwa kwenye hospitali 22 zinazosaidiwa na mradi wa kujenga uwezo wa CCBRT.

Mshauri wa kiufundi wa mradi wa kujenga uwezo wa CCBRT, Dk Brenda Sequeira D’mello, alisema: “Mpango huu wa kuzipatia hospitali mashine za Utrasound ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa miaka saba wa kuwajengea uwezo watumishi wa afya na kuboresha miundombinu ya afya katika hospitali na vituo vya afya 22 nchini unaoendeshwa kwa pamoja kati ya CCBRT na timu ya afya ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Mashine hizi ni zawadi kwao kwa kuwa wameweza kufikia vigezo kwa kuboresha huduma za uzazi na mtoto Dar es Salaam,” alisema D’mello.