Tuesday, January 16, 2018

Hospitali iliyoanza kujengwa mwaka 1980, sasa kumaliziwa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mara. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati akikagua ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kuwasili mkoani Mara kwa ajili ya ziara yake ya kikazi akisema Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa awamu na wataanza na eneo la mapokezi na vyumba vya madaktari.

Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo anawaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu alisema tayari Serikali imeshatoa Sh1.4 bilioni ili ujenzi uendelee. Ujenzi huo ulianza mwaka 1980, ulisimama mwaka 1987 na kuanza tena 2010.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alikagua Uwanja wa Ndege wa Musoma mkoani Mara ambao unatarajiwa kukarabatiwa na kuwekwa lami.

Alisema kukamilika kwa ukarabati huo wa uwanja kutafungua fursa za utalii ndani ya mkoa huo ambao umezungukwa na vivutio vingi.

Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kukarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwamo cha Musoma ili kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kukarabatiwa ni Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea.

Waziri Mkuu alisema viwanja hivyo kwa sasa vinakarabatiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ambao wanajenga kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyostahili.

Awali, Meneja wa Tanroads, Mkoa wa Mara, Mlima Ngaila alisema ukarabati huo utafanyika kwa awamu tatu, ya kwanza itahusisha upanuzi wa uwanja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Alisema barabara ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa kilomita 1.6 na upana wa mita 33, ni ya changarawe, hivyo kusababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma na kuridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 kongwe nchini ambazo Serikali iliamua kuzikarabati ili ziweze kurudi kama zamani na kuendelea kutumika.     

-->