Hospitali ya Mkapa sasa kupandikiza figo

Muktasari:

Hayo yamethibitishwa jana Januari 20, 2018 na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chanika kwenye hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya hospitali hiyo na Udom.

Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa Ultra Modern iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) itaaanza kutoa huduma ya kwanza ya kupandikiza figo  Machi mwaka huu.

Hayo yamethibitishwa jana Januari 20, 2018 na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chanika kwenye hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya hospitali hiyo na Udom.

“Tuna vifaa na mashine za kisasa kabisa kwa ajili ya upandikizaji wa figo. Mwezi Machi mwaka huu tutaanza na  wagonjwa wawili ambao tutawafanyia tayari wapo na kinachosubiriwa ni siku tu ifike,” amesema na kuongeza,

"Upandikizaji wa figo nchini ni teknolojia ngeni kidogo ndiyo maana nasema utakuwa ni wa kihistoria na utafanywa na madaktari wa Tanzania kwa kushirikiana na wenzao kutoka Japan kwa kuwa wenzetu wameanza siku nyingi na siyo kitu kipya kwao kama ilivyo hapa kwetu."

Amesema upandikizaji huo utafanyika bure kwa kuwa hospitali hiyo na Udom zitagharamia gharama za matibabu.

"Tuna wagonjwa wawili tutakaowapandikiza figo na gharama zao zitalipwa na chuo na hospitali hii kwa sababu mpaka sasa gharama halisi ya kufanya upandikizaji wa figo bado haijapangwa  mpaka wizara ya afya itakapotangaza. Naamini haitakuwa kubwa,” amesema.

Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Idris Kikula amesema, “Tunajua wenzetu wa Muhimbili walifanya upandikizaji wa figo kwa mafanikio makubwa sana na sisi tumejipanga mwezi Machi mwaka huu tutafanya kwa mara ya kwanza.”

Amesema matibabu hayo yatawapa nafuu wananchi na wakazi wa Dodoma kwa maelezo kuwa sasa hawatalazimika kwenda nje ya nchi.