Hospitali ya Mount Meru Arusha yasaidiwa mtambo wa sola

Meneja wa Kampuni ya Mobisal Kanda ya Kaskazini,  Stephens Kangala akimkabidhi mtambo wa umeme wa jua Muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mountmeru  Sifaeli Masawe jana wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi na kutoa damu. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  •         Mahitaji ya damu katika hospitali hiyo ni chupa 450 kwa mwezi, lakini wamekuwa wakipata chupa 150 tu

Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru imepokea msaada ya mtambo wa umeme wa jua (sola) na vifaa vya usafi vyote vikiwa na thamani ya Sh6 milioni.

Msaada huo ulitolewa jana na Kampuni ya Mobisol ili kuondoa adha ya kukosekana umeme katika wodi ya kinamama na watoto.

Meneja wa Mobisol Kanda ya Kaskazini, Stephen Kangala alisema kampuni yao ambayo inajihusisha na usambazaji wa umeme wa jua, imetoa msaada huo ili kusaidia wagonjwa wanaopata tiba hospitalini hapo.

Alisema sambamba na msaada wa mtambo wa sola ambao hutumika kwa wodi zaidi ya tatu, pia wametoa vifaa vya usafi na wafanyakazi kuchangia damu.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Sifaeli Masawe alishukuru Kampuni ya Mobisol kwa msaada huo.

Masawe alisema msaada huo utasaidia sana kupunguza tatizo la kukosekana umeme hasa wakati wa kujifungua wajawazito na kwenye chumba cha upasuaji.

Pia, aliwashukuru wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kujitolea damu kwa kuwa hospitali hiyo mara kadhaa imekuwa ikikabiliwa na tatizo la upungufu wa damu.

Alisema mahitaji ya damu katika hospitali hiyo ni chupa 450 kwa mwezi lakini wamekuwa wakipata chupa 150 tu. Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru imekuwa ikitumika kama hospitali ya rufaa kutokana na kupokea wagonjwa wengi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani.