Hospitali zote za Marie Stopes Tanzania zapigwa ‘stop’ kwa kukiuka miongozo

Muktasari:

Serikali yasema kufungiwa kwa zaidi ya wiki tatu sasa kunatokana na ukiukaji wa miongozo, yasubiri taarifa kamili ili itoe taarifa kwa umma juu ya sakati hilo
    

Dar es Salaam. Baada ya kuibuka kwa sintofahamu takriban wiki tatu tangu hospitali na zahanati za Marie Stopes Tanzania (MST), zisimamishe huduma, hatimaye imethibitika kuwa zimepigwa ‘stop’ na Serikali.

Wiki iliyopita, uongozi wa taasisi hiyo kupitia kwa ofisa uhusiano wao, Dotto Mnyadi uliliambia Mwananchi kuwa kusimamishwa kwa huduma kulitokana na ukaguzi uliokuwa ukifanywa na Serikali pamoja na ukarabati.

Hata hivyo, jana naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayehusika na masuala ya Afya, Josephat Kandege alisema Marie Stopes imesitishiwa kutoa huduma kwa sasa kutokana na kukiuka miongozo.

“Mhusika ambaye atakuwa kwenye nafasi nzuri kuweza kulizungumzia hili ni mganga mkuu wa Serikali ili tuwe na taarifa sahihi kuitaarifu jamii,” alisema Kandege.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, mganga mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi simu yake ya kiganjani haikupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu. Vituo vilivyofungiwa vipo Arusha, Mwanza, Musoma, Iringa, Mbeya, Kahama, Temeke, Kimara, Mabibo na Hospitali ya Mwenge isipokuwa kituo cha Zanzibar.