Huduma za fedha kwa njia ya mtandao zilivyogeuka mkombozi kwa wanawake

Muktasari:

  • “Kuna wakati nilipoteza simu yangu, niliogopa sana nilijua huo sasa ndiyo mwisho wangu lakini hali ikawa tofauti na baada ya kutoa taarifa katika kampuni ya simu na kunirejeshea huduma fedha zangu zote zilirejea,” anasisitiza Sikujua.

Awali ilinilazimu kuhifadhi fedha zan-gu chini ya godoro kwa kuwa sikuwa na akaunti benki nakumbuka siku moja moto uliwaka nyumbani kwangu na kuteketeza kila kitu wakati nikiwa katika biashara zangu.”Ni maneno ya Sikujua Athumani mkazi wa kijiji cha Kidomole Bagamoyo ambaye ni mfanyabiashara wa samaki katika soko kuu la samaki Bagamoyo.

Sikujua anasema tukio hilo lilimrudisha nyuma na kwa zaidi ya miezi sita ilimlazimu kukaa nyumbani ili kukusanya mtaji mwingine ambako alilazimika kufanya vibarua vya kulima kwa ujira mdogo.“Laiti huduma za fedha kwa njia ya mitandao ya simu ingekuwapo wakati huo nisingeteseka, kwa sasa fedha zangu zote baada ya mauzo yangu ya samaki naziweka katika akaunti yangu ya mtandao wa simu na kutumia kido-go kidogo,”anasisitiza.Sikujua ambaye ni mama wa wato-to watano anasema; “wakati fedha zake zikiungua hakuwa na akaunti benki kwa sababu tu hakuweza kutimiza masharti.

Lakini sasa Sikujua suala la kuhofia kupoteza fedha zake limekuwa historia kutokana na ukweli kwamba ama halazimiki kutembea na fedha taslimu au kuzificha chini ya mchago.

“Kuna wakati nilipoteza simu yangu, niliogopa sana nilijua huo sasa ndiyo mwisho wangu lakini hali ikawa tofauti na baada ya kutoa taarifa katika kampuni ya simu na kunirejeshea huduma fedha zangu zote zilirejea,” anasisitiza Sikujua.

Anasema mitandao hiyo imeinua maisha yake, amefanikiwa kujenga, kusomesha watoto lakini pia sasa anaweza kutatua masuala ya kifamilia bila msaada wowote tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Sasa watoto wangu nawalipia ada kwa wakati na pia nimeweza kumudu maisha kwa kuwa nina uhakika wa chakula lakini pia nimekuwa msaada mkubwa wa wazazi wangu,” anasisitiza Sikujua.

“Kifupi imenifanya niwe mwanamke ninayejitimizia matatizo yangu kwa kushirikiana na mume wangu ambaye naye anajishughulisha na biashara za kusafiri,”anasisitiza.

“Fedha ninazopata pia zimenisaidia kununua shamba ambalo nimejenga mabanda kwa ajili ya ufugaji wa kuku ambako sasa wamefika 1,500.”

Anaongeza kuwa kutokana na kutumia huduma hizo za kifedha kupitia mitandao ya simu hata anapohitaji kununua mahitaji kwa ajili ya biashara zake kama vyakula vya kuku hutuma moja kwa moja badala ya kulazimika kutembea na fedha.

Hata hivyo, Sikujua anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni utapeli na wizi; “mara kwa mara wanafika matapeli wanaturubuni usipokuwa makini unaweza kupoteza fedha nyingi sana,” anasisitiza.

Mwantumu Zembwela naye anasema kuwa huduma hizo za kifedha zimemuwezesha kujiajiri na kujiongezea kipato.

“Awali nilikuwa mama wa nyumbani baadaye nikamuomba mume wangu anipatie mtaji akanipatia Sh500,000 ambazo nilianza kutoa huduma ya kutoa na kuweka fedha kwa mitandao yote na hivi ninavyoongea mtaji wangu umekuwa mpaka kufikia Sh2 milioni,” anaongeza.

Mwantumu anasema huduma hizo zimemsaidia kujikwamua na umaskini na kumuongezea kipato cha familia lakini pia kuongeza pato la Taifa kwa kuwa sasa ni mlipa kodi mzuri.

“Sasa nimeweza kuajiri kijana mmoja ambaye ninamlipa kiasi cha Sh20,000 kwa mwezi awali sikuwahi kufikiri kwamba ipo siku nami nitakuwa mwajiri lakini kubwa zaidi nalipa kodi ya biashara kwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA),” anasisitiza.

Jamila Hussein mkazi wa Fukayosi, Pwani yeye anasema huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu zimemsaidia mtaji wa kuanzisha biashara yake ya kuuza vipodozi.

“Natumia huduma ya mtandao, nilijiwekea malengo ya kupata fedha nyingi kwa pamoja ili zinisaidie kuanzisha biashara yangu nashukuru baada ya miezi mitatu nilifanikisha hilo,” anasisitiza.

Jinsi teknolojia ilivyobadili maisha

Teknolojia ya huduma za kifedha kwa mitandao imeleta mapinduzi makubwa duniani. Imerahisisha mambo na kuinua uchumi, imesogeza mawasiliano karibu na kupunguza muda uliotumika zamani na kuongeza urahisi wa kutuma na kupokea fedha.

Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha idadi ya watumiaji wa mitandao hapa nchini ilifikia watu milioni 23 jambo lililorahisisha mawasiliano ya kibiashara, huku watumiaji wengine wakinufaika kwa kupata ajira.

Bulaya awapa somo wanawake

Mbunge wa Bunda mjini Esther Bulaya anasema utaratibu wa kina mama wengi kuhifadhi fedha chini ya godoro au katika vyombo maalumu ikiwamo kufukia chini ya ardhi si salama.

Bulaya anawataka wanawake kutumia huduma hizo kwa manufaa yao na kuhakikisha wanaepuka utapeli ambao unaonekena ndiyo changamoto kubwa.

“Hakuna asiyejua sasa wanawake wamegeuka injini ya familia nyingi, ndiyo wanaofanya biashara na kulisha na kuwapeleka shule watoto, ujio wa mitandao hii utawasaidia kuondokana na umaskini uliokithiri,”anasisitiza.

Bulaya anasema hata katika jimbo lake wapo wanawake wanaojishughulisha na wamefanikiwa kujiajiri kupitia mitandao hiyo lakini wapo pia walioajiri wengine.

Tanzania yaongoza huduma za kifedha

Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza duniani kufanikiwa katika utoaji wa huduma za kifedha kwa kutumia mitandao ya simu.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Injinia James Kilaba anasema: “Huduma za kifedha kwa mfumo wa digitali nchini Tanzania imepiga hatua kubwa ukilinganisha na nchi nyingine duniani.

Injinia Kilaba ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa wadau wa mawasiliano ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) kwa kushirikiana na TCRA anasema awali wananchi hawakuwa na uelewa wa matumizi ya huduma hizo lakini sasa hali imebadilika na kuzipita nchi nyingi duniani.

Faida za huduma za kifedha

Kwa mujibu wa taarifa za Tovutipoa, huduma za fedha kwa njia ya mtandao imewezesha taasisi mbalimbali kuwakopesha fedha watumiaji wa simu hizo kwa vigezo nafuu.

Taasisi hizo zinatoa mikopo yenye masharti nafuu ambayo viwango vyake vinaanzia Sh5,000 hadi milioni kadhaa kutegemea na vigezo vilivyowekwa na wamiliki wa taasisi hizo ikiwamo urejeshaji wa mikopo kwa wakati.

Ili unufaike na mikopo hiyo unapaswa kuwa na simu janja (smartphone) ambapo utapakua App ya taasisi utakayoipenda kisha utafungua akaunti yako kwenye app hiyo.

Taasisi kadhaa zikiwapo Tala inayotoa huduma ya mikopo katika nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Mexico, Tanzania na Ufilipino.

Nyingine ni matawi ambayo pia yanatoa mikopo rahisi na nafuu kupitia mitandaoni kwa kutumia simu.

Mikopo hii inawafaa wajasiriamali wadogo wadogo ambao hawana vigezo vya kukopa fedha nyingi katika taasisi kubwa za kifedha.

Kadri unavyokopa na kurejesha mikopo kwa wakati, ndivyo unavyojiongezea nafasi ya kukopeshwa pesa nyingi zaidi.