Hukumu kesi ya Masogange Februari 21

Muktasari:

Akiongozwa na mawakili Nehemiah Nkoko na Ruben Simwanza kutoa utetezi wake leo Februari 15, 2018 Masogange ameiomba mahakama hiyo imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.

 


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema Februari 21,2018 itatoa hukumu kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili msanii, Agnes Gerald maarufu Masogange.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Costantine Kakula kuwaita mashahidi watatu kutoa ushahidi dhidi ya Masogange na kuufunga na mshtakiwa kujitetea mwenyewe.

Akiongozwa na mawakili Nehemiah Nkoko na Ruben Simwanza kutoa utetezi wake leo Februari 15, 2018 Masogange ameiomba mahakama hiyo imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.

Masogange ambaye anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam, katika utetezi wake amedai kuwa yeye hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja.

Ameiambia mahakama kuwa mbali ya usanii, alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo.

Alidai kuwa Februari 14,2017 polisi walikwenda nyumbani kwake bila yeye kuwapo kwa sababu alikuwa amempeleka mjomba wake Ocadeco kununua, hivyo walimkuta dada yake.

"Polisi waliniulizia, dada yangu aliwauliza nyie ni kina nani, wakamueleza kuwa wao ni ndugu zetu, dada yangu aliwaambia sisi hatua ndugu kama nyie," ameeleza Masogange.

Ameeleza kuwa polisi hao walimweka chini ya ulinzi dada yake na kumtaka ampigie simu ajifanye anaumwa ili arudi nyumbani.

Masogange ameeleza kuwa Sada yake alimpigia simu na kumweleza anaumwa sana, naye akamjulisha kuwa atarejea nyumbani muda si mrefu lakini alikwenda saa 12:00 jioni.

Amedai kuwa ilipofika nyumbani kwake getini kabla hajashuka kwenye gari, alimuona mlinzi amekaa na watu wanne, aliwasalimia na kuingia ndani.

Amedai kuwa ilipofika ndani alimkuta dada yake, askari wa kike na askari wawili wa kiume, walimweleza wanamsubiri yeye na wakajitambulisha kuwa wao ni polisi.

Masogange alidai kuwa aliwauliza shida yao na kumweleza kuwa wamekwenda kufanya upekuzi, lakini hawajapata kitu chochote.

Amedai baada ya upekuzi huo, walimchukua na kupeleka Kituo Kikuu cha Polisi na walipofika mapokezi akaandikisha jina na wakampeleka rumande ambako alikaa siku tisa.

Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa Februari 14,2017, Februari 15,2017 akiwa polisi alipelekwa katika ofisi iliyokuwa na watu 15, ambako kwa nyakati tofauti alikuwa wakimuuliza maswali.