Hukumu kesi ya Wema yaanza kusomwa

Muktasari:

Hukumu hiyo ilipaswa kusomwa Julai 16, 2018 lakini ilisogezwa mbele hadi leo kutokana na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba anayesikiliza shauri hilo kutokamilisha kuandika hukumu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Julai 20, 2018 imeanza kusoma hukumu ya kesi ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili.

 

Hukumu hiyo ilipaswa kusomwa Julai 16, 2018 lakini ilisogezwa mbele hadi leo kutokana na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba anayesikiliza shauri hilo kutokamilisha kuandika hukumu.

 

Leo hakimu Simba ndio anayesoma hukumu hiyo.

 

Mbali na Wema washtakiwa wengine ni wafanyakazi wake; Angelina Msigwa (23) na Matrida Abas (19).

 

Awali, Wema alikubali nyumbani kwake kulikuwa na msokoto unaodhaniwa ni bangi, vipisi ambavyo hajui ni kitu gani katika chumba cha kuhifadhia nguo zake, pochi, viatu na kibriti katika chumba wanacholala wanamuziki wawili Jordan na Mila.

 

Akiongozwa na wakili Albert Msando kujitetea, Wema alieleza kuwa yeye hajui mmiliki wa vitu hivyo kwa sababu yeye ni msanii wa filamu na nyumbani wake wanaingia watu tofauti tofauti.

 

Amedai kawaida huwa anafanya sherehe na kualika watu katika nyama choma na chakula cha mchana.