IGP Sirro alipongeza Jeshi la Polisi Singida

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro

Muktasari:

IGP Sirro ametoa pongezi hizo leo asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kweye viwanja vya kambi ya Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU) mjini  hapa.

Singida. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani Singida kwa juhudi zake za kupunguza matukio ya uhalifu yakiwamo ya utekeji wa magari.

IGP Sirro ametoa pongezi hizo leo asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kweye viwanja vya kambi ya Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU) mjini  hapa.

Amesema matukio ya uhalifu mbalimbali mkoani Singida yamekuwa yakipungua kwa kiwango kikubwa kwa  sasa, ikilinganishwa na miaka ya  nyuma.

“Hatua hii  inachangia  uwepo  wa amani  na utulivu kwa wananchi wa mkoa wa Singida hivyo kutoa fursa za kujiletea maendeleo yao ya mkoa na  taifa  kwa ujumla,” amesema.

IGP Sirro amesema mafanikio hayo yamechangiwa   na wananchi kwa kiwango kikubwa kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Jeshi la Polisi. 

Akifafanua amesema wananchi wamekuwa wakitoa  taarifa sahihi na kwa  wakati kwa Jeshi la Polisi  pindi wanapobaini dalili ama matukio ya kihalifu.

“Kwa sasa kwa kweli wananchi hata ninyi waandishi  mnatupa  ushirikiano  mzuri ambao unachangia kazi zetu kuwa nyepesi na za mafanikio makubwa. Sasa  kule Kibiti mkoani Pwani, wananchi wanatusaidia mno taarifa zinazohusu mauaji ya watu wasiokuwa  na hatia,” amefafanua zaidi.

IGP Sirro amesema kwa sasa Tanzania inaonewa wivu na nchi jirani kwa namna ilivyodhibiti matukio ya kihalifu na kupelekea nchi kuendelea kudumisha amani na utulivu.

Wakati huo huo, IGP Sirro ametumia fursa hiyo  kuwaomba wananchi waendelee kushirikiana na jeshi hilo, kufichua baadhi ya watu wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki.