VIDEO-IGP Sirro ataka mwenye taarifa za Azory kuzipeleka

Muktasari:

  • Sirro alisema wanalifuatilia suala hilo ili kubaini alipo, lakini wanahitaji ushirikiano kutoka kwa watu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema uchunguzi kuhusu kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti hili, Azory Gwanda unaendelea hivyo mtu yeyote mwenye taarifa au atakayesikia kuhusiana na mwandishi huyo asisite kulifahamisha jeshi hilo.

Sirro alisema wanalifuatilia suala hilo ili kubaini alipo, lakini wanahitaji ushirikiano kutoka kwa watu.

Gwanda ambaye kituo chake cha kazi ni Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Novemba 21, 2017 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa Kibiti majira ya saa 4:00 asubuhi.

Licha ya jitihada za kutangaza na kulaani kutoweka kwake, hadi jana zimetimia siku 84 hakuna taarifa kamili zinazoelezea alipo.

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya kumuapisha Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Hassan Haji, Sirro alisema jalada la uchunguzi kuhusu kutoweka kwa Gwanda lipo na wanaendelea kulifanyia kazi.

Alisema wanaendelea kukusanya taarifa hivyo atakayesikia chochote kuhusu mwandishi huyo asisite kulifahamisha jeshi hilo na taarifa zake zitafanyiwa kazi. “Tunaendelea kukusanya taarifa, ushahidi kuhusiana na kutoweka kwa Gwanda, hivyo mwananchi mwenye taarifa asisite kutuletea zitakuwa siri kati yetu na yeye na tutazifanyia kazi kuhakikisha mwandishi huyo anapatikana,” alisema.

Naye katibu wa mawasiliano wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu aliiomba Serikali itoe taarifa ya uchunguzi kuhusu kupotea kwa mwandishi huyo aliyefikisha siku ya 85 leo tangu kupotea kwake sanjari na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo, Simon Kanguye.

Katika hatua nyingine, Shaibu alisema kuanzia sasa chama hicho kitakuwa kinajibu ripoti zote kuhusu mwenendo wa Serikali zitakazokuwa zikitolewa na msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas.

Changamoto za polisi

Sirro alielezea changamoto zinazolikabili Jeshi hilo ikiwamo ucheleweshaji wa kesi, viashiria vya ugaidi na rushwa. Alisema Jeshi hilo lina kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utulivu.

Alimtaka Kamishna Haji kuzifanyia kazi changamoto hizo kwa uadilifu mkubwa, ikiwamo kupambana na viashiria vya ugaidi vinavyojitokeza kwenye matukio kadhaa ya kihalifu.

Naye Kamishna Hajji alisema amevisikia vipaumbele anavyotakiwa kuvifanyia kazi na yupo tayari.

Alishukuru maelekezo, mwongozo aliokuwa akipewa na IGP ambao umemfikisha katika cheo hicho.