IGP Sirro awaomba viongozi wa dini kuhubiri amani ili mauaji yakome

Muktasari:

  • Alisema hayo juzi alipojibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua mikakati ya jeshi hilo katika kukabiliana na mauaji mkoani humo.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amewaomba viongozi wa dini mkoani Rukwa kuongeza bidii katika kuhubiri amani ili mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na wivu wa mapenzi yapungue mkoani humo.

Alisema hayo juzi alipojibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua mikakati ya jeshi hilo katika kukabiliana na mauaji mkoani humo.

IGP Sirro alisema Jeshi la Polisi linajitahidi kukabiliana na mauaji yote yanayotokea nchini lakini katika mkoa huo takwimu zinaonyesha mauaji yanayotokana na ushirikina na wivu wa mapenzi yanaongoza.

Alisema viongozi wa dini wana jukumu kubwa katika kuhakikisha wanahubiri amani ili mauaji hayo yapungue kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kuwalea wananchi kiroho.

“Napenda kuwaomba viongozi wa dini wahusike kikamilifu katika vita ya kumaliza mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi, na wananchi kabla ya kufanya vitendo hivyo, ni lazima watafakari kwa kuwa mtu ukiua unahukumiwa kunyongwa, unawaacha watoto wako yatima na kuwaharibia maisha, hivyo watakosa malezi ya wazazi,” alisema.

IGP Sirro aliahidi kuwa jeshi lake kupitia bajeti zake, litajenga kituo kipya cha polisi Sumbawanga mjini kwa kuwa kilichopo ni kimechakaa na majengo yanayotumika yalirithiwa kutoka Shirika la Reli Tanzania.

Pia, aliahidi kuupatia Mkoa wa Rukwa gari jipya litakalotumika katika matumizi ya polisi kwa kuwa kuna upungufu wa vitendea kazi.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi na kubadilika kwa kuacha kubweteka kwa kuwa maisha yamekuwa tofauti.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alimweleza IGP Sirro kuwa kuna mpango wa kuanza mchakato wa kujenga nyumba za kuishi askari kwa kushirikiana na wafanyabiashara ili kupunguza mahitaji ya makazi ya watumishi hao.

Alisema askari wengi wanaishi uraiani na baadhi hupoteza weledi wa kazi yao.