IGP Sirro awatangazia kiama wanaoingiza silaha, wakimbizi

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro akiwagawia mahindi wananchi baada ya kumaliza kusalimiana nao wakati akitokea mkoani Tabora kwenda mkoa wa Kigoma katika ziara ya kikazi, juzi.  Picha na Jeshi la Polisi

Muktasari:

  • Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, jeshi hilo linafuatilia kwa makini mienendo ya wanaodaiwa kuwamo kwenye mtandao wa kuingiza wahamiaji haramu na biashara ya silaha kutoka nchi jirani.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewaonya wakazi wa mikoa ya mipakani kujiepusha na tabia ya kukaribisha raia wa kigeni na kuwatumikisha mashambani huku wakifanya biashara haramu ikiwamo ya silaha.

Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, jeshi hilo linafuatilia kwa makini mienendo ya wanaodaiwa kuwamo kwenye mtandao wa kuingiza wahamiaji haramu na biashara ya silaha kutoka nchi jirani.

“Wapo Watanzania wanaojihusisha na mtandao wa biashara haramu ya silaha wakishirikiana na wakimbizi wanaoingia nchini kinyume cha sheria, siku zao zinahesabika,” alisema.

IGP alisema mikakati ya kudhibiti mitandao ya kihalifu inahusisha nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashari na Kati. “Tunatarajia kusaini makubaliano na Jeshi la Burundi kuwezesha operesheni ya pamoja kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka ikiwamo uingiaji holela wa wanaojiita wakimbizi ambao wanajihusisha na biashara ya kuuza silaha,” alisema.

Akizungumzia mkakati huo, mkazi wa Ujiji Kigoma, Zuwena Abdallah alisema kwamba polisi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wanapaswa kuimarisha udhibiti na ukaguzi maeneo ya mipakani.

Kiongozi huyo wa polisi alitembelea Kigoma kukagua shughuli na utendaji wa jeshi hilo.