IGP amsubiri Rais kuhamia Dodoma

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu

Muktasari:

Wananchi wana imani kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) atakapohamia Dodoma usalama utaimarika

Dodoma. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu huenda akachelewa kuhamia makao makuu ya nchi mjini Dodoma tofauti na ilivyotangazwa awali.

Awali jeshi hilo liliweka mpango wake wa kuhamia Dodoma kabla ya Rais John Magufuli kuhamia, lakini kwa sasa kiongozi huyo atawasili mjini hapa baada ya Rais kuwasili.

Imeelezwa kuwa IGP Magu akifika Dodoma, makao makuu yake yatakuwa eneo la Nzuguni nje kidogo ya mji huo.

Awali makao makuu ya jeshi hilo yaliripoti kuhamia Dodoma Agosti kabla ya kubadili uamuzi huo kwa lengo la kusubiri mkuu wa nchi kuhamisha makazi yake kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Chamwino.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, jana alisema maandalizi ya awali yamekamilika na kuwa akifika IGP ataanzia kazi katika jengo la Kamanda wa Polisi wa mkoa huo.

Kamanda Mambosasa alisema kazi iliyopo sasa ni kuendelea kuijenga Dodoma yenye amani ili iendelee kustawi zaidi kwa sababu kutakuwa na ongezeko kubwa la watu jambo linaweza kuchangia kuongezeka kwa uhalifu.

Eneo analotarajia kuhamia IGP Mangu, linapatikana pembezoni mwa mji wa Dodoma takriban kilometa 10 kutoka mjini ambako zamani lilielezwa kuwa ni sehemu inayotarajiwa kujengwa Chuo Kikuu cha Polisi na lipo katikati ya kijiji cha Nzuguni na Ihumwa likipakana na uwanja wa maonyesho ya wakulima ya Nanenane.

Wakazi wa Nzuguni walisema kitendo cha IGP Magu kuhamia eneo hilo ni ishara kwamba eneo hilo sasa itakuwa salama zaidi kuishi.

Mwendesha bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Makole alisema kuhamia kwa IGP Dodoma kutasababisha wafanye biashara zao katika hali ya usalama kwa kuwa wanaamini hali ya ulinzi itaimarishwa.

“Kwa mfano sasa tunaogopa kuendesha bodaboda ikifika usiku, lakini kama ulinzi ukiimarishwa ni wazi kwamba hofu hiyo itapungua na miundombinu kama barabara itaboreshwa ili iwe rafiki katika biashara zetu,” alisema Makole.