IGP mstaafu Uganda alaani ukomo wa rais kuondolewa

Muktasari:

  • Ataka wajikite kushughulikia matatizo kama njaa na umaskini
  • Kwamba wanaounga mkono hoja hiyo wana mawazo finyu
  • Hizo ni salamu kwa wabunge wa chama cha NRA na mawaziri 23

Inspekta Jenerali Mstaafu (IGP), Julius Odwe ameongeza uzito katika sauti zinazolaani pendekezo la kufutwa Ibara ya 102 (b) ya Katiba, iliyoweka ukomo wa umri wa rais kuwa miaka 75

Katika taarifa yake iliyotolewa asubuhi leo Odwe anasema uamuzi wa baadhi ya wabunge wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na mawaziri 23 kutaka kufuta ukomo wa umri wa rais siyo tu kwamba unaudhi bali pia inaonyesha wana mawazo finyu.

Ofisa huyo wa zamani wa ngazi ya juu anasema Waganda wanakabiliwa na matatizo mengi mazito yanayohitaji kushughulikiwa haraka kuliko kukaa kufikiria kuondoa ukomo wa umri wa rais na kurejeshwa kwa nguvu ardhi serikalini mambo ambayo serikali imeamua kujikita.

Alielezea hofu waliyonayo Waganda kuhusu uongozi wa mpito na mrithi wa Rais Museveni, hofu ya utumishi dhaifu katika sekta ya umma, njaa, umaskini na ukosefu wa haki vyote vikihitaji hatua za haraka.

Odwe alitupilia mbali hoja ya wanaoshinikiza kuondolewa kwa ukomo wa rais kwamba inalenga kuhakikisha vijana, ambao idadi yao ni asilimia 80 ya Waganda, wanapata fursa ya kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, akisema hakuna uwezekano wa kijana kuja kuwa rais wa Uganda.

Odwe alisema katika historia, ni vijana kumi tu waliowahi kufanikiwa kuwa wakuu wa nchini barani Afrika tangu mwaka 1960 tena kupitia mapinduzi ya kijeshi au kurithishwa. Amewataja baadhi ya vijana hao kuwa ni Kanali Muammar Gaddafi aliyetawala Libya baada ya kufanya mapinduzi akiwa na miaka 27 mwaka 1969 na Yahya Jammeh wa Gambia aliyetawala akiwa na miaka 29 baada ya mapinduzi mwaka 1994.

Wengine ni Joseph Kabila wa DR Congo, Valentine Strasser wa Sierra Leone na Michael Micombero aliyetawala Burundi akiwa na umri wa miaka 26 kuanzia mwaka 1966.