IPTL yaungana na Tanesco uamuzi wa ICSID

Muktasari:

Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) iliyopo nchini Uingereza, imeitaka Tanesco kuilipa benki ya Standard Chartered zaidi ya Sh320 bilioni pamoja na riba kama gharama za uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme.

Dar es Salaam. Mwanasheria na mshauri mkuu wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Joseph Makandege amesema kampuni hiyo inaunga mkono hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukata rufaa kupinga kuilipa benki ya Standard Chartered zaidi ya Sh320 bilioni.

Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) iliyopo nchini Uingereza, imeitaka Tanesco kuilipa benki ya Standard Chartered zaidi ya Sh320 bilioni pamoja na riba kama gharama za uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme.

Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco imeeleza dhamira yake ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama. Imesema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uendeshaji wa mahakama tangu kesi ilipofunguliwa mwaka 2010.

IPTL imesema haiitambui benki ya Standard Chartered - Hong Kong kama mdai wake, na kwamba haina haki ya kupata malipo yoyote kwa niaba ya kampuni hiyo.

Mgogoro kati ya IPTL na benki hiyo umeibuka upya baada ya mahakama ya ICSID kuitaka Tanesco kuilipa kwa niaba ya IPTL kwa sababu ilinunua deni la kampuni hiyo.