Wanafunzi waliopoteza maisha wafikia 6, majeruhi 42

Muktasari:

Mganga Mkuu  Hospitali ya Rulenge Sr Goleth Fredrick amesema idadi hiyo imeongezeka baada ya wengine kutolewa katika kituo cha afya Bukiriro na kwamba wanafunzi watatu wamefariki na kufikisha idadi ya vifo vya wanafunzi sita.

Ngara. Idadi ya wanafunzi waliopoteza maisha  kutokana na bomu la  kutupwa kwa mkono katika shule ya msingi Kihinga wilaya ya Ngara mkoani Kagera imeongezeka na kufikia sita huku kukiwa na majeruhi  42 ambao wamelazwa Hospitali ya misheni Rulenge.

Mganga Mkuu  Hospitali ya Rulenge Sr Goleth Fredrick amesema idadi hiyo imeongezeka baada ya wengine kutolewa katika kituo cha afya Bukiriro na kwamba wanafunzi watatu wamefariki na kufikisha idadi ya vifo vya wanafunzi sita.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Agustino Olomi amesema chanzo cha wanafunzi hao kujeruhiwa kwa bomu ni baada ya mmoja wao kuliokota akidhani ni chuma chakavu.

“Mmoja wapo aliliokota akidhani kwamba ni chuma chakavu hivyo akaamua kuja nalo shuleni baadaye  alipeleke kwa mnunuzi  ili aweze kununua  madaftari’’amesema

Hata hivyo kamanda wa Kikosi cha Kulinda mipaka cha jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ wilaya ya Ngara meja Mutaguzwa amesema bomu hilo lilikuwa na vipande 36 na lingelipukia ndani ya darasa lingeleta athari zaidi .

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Rulenge, Goreti Francis amethibitisha kupokewa miili  ya wanafunzi hao  waliopoteza maisha.

“Majeruhi wana majeraha sehemu mbalimbali za mwili, tunafanya kila jitihada kuokoa maisha yao,” amesema Dk Francis.

Akizungumza kwa simu akiwa eneo la tukio, zaidi ya kilomita 50 kutoka Ngara mjini, diwani wa Kibogora, Adronis Bulindoli amesema wanafunzi waliofariki wana umri kati ya miaka minane na tisa.