Wizara yazungumzia idadi ya wakunga, wauguzi

Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga wa wizara, Gustav Moyo 

Muktasari:

Wanafunzi kati ya 2,500 na 3,000 humaliza masomo ya ukunga na uuguzi kila mwaka.

Dodoma. Wizara ya Afya imesema kuna safari ndefu ya kuwa na wakunga na wauguzi wanaotosheleza mahitaji kwa kuwa waliopo sasa ni asilimia 55.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Shirika la Utafiti na Tiba barani Afrika (Amref) na wizara, mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga wa wizara, Gustav Moyo amesema mikakati ambayo Serikali imechukua ni kuongeza idadi ya wanafunzi katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya uuguzi na ukunga.

Amesema wanafunzi kati ya 2,500 na 3,000 humaliza masomo kila mwaka.

“Changamoto kubwa ilikuwa ajira kwa sababu ya uhakiki wa vyeti na wafanyakazi hewa lakini baada ya kipindi kifupi vibali vya ajira 3,000 vilitolewa na kama alivyoahidi Rais (Dk John Magufuli) vitapatikana vibali zaidi vya ajira katika sekta hii,” amesema.

Amesema baadhi ya wauguzi wamekuwa hawatoi huduma kwa kuzingatia maadili, utu na heshima.

Moyo amesema Serikali imechukua hatua kwa kuandaa miongozo ya mafunzo ambayo husaidia kuwakumbusha mambo hayo.

Meneja mradi wa ukunga salama wa Amref, AnnaGrace Katembo amesema unatekelezwa katika wilaya 19 nchini na unalenga kuangalia idadi ya wauguzi na wakunga waliopo na kushirikishana taarifa na wadau.

“Tunafanya kazi pia na Wizara ya Elimu ili kuhamasisha wanafunzi wengi wafikie vigezo vya kujiunga na mafunzo ya ukunga na uuguzi,” amesema.