Ilani ya CCM yaibua mzozo kikaoni

Muktasari:

Tukio hilo lilitokea jana Jumanne walipokutana kujadili na kupitia bajeti ya jiji ya mwaka 2015/16 na 2016 /17.

Dar es Salaam. Kauli kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani jijini hapa imeibua mvutano kati ya wajumbe wa chama hicho na wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Tukio hilo lilitokea jana Jumanne walipokutana kujadili na kupitia bajeti ya jiji ya mwaka 2015/16 na 2016 /17.

Mvutano huo ulimlazimu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kutumia busara kuwatuliza wajumbe hao.

Ilivyokuwa

Mwita alimpa nafasi ya kuchangia mjumbe wa CCM ambaye pia ni Diwani wa Kibonde Maji, Abdallah Mtinika ambaye alisema: “Ahsante mheshimiwa mwenyekiti, nakupongeza kwa kuongoza vyema jiji hili na mambo yanakwenda vizuri. Hii inaonyesha jinsi unavyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015-20.”

Maelezo hayo yalisababisha mwenzake wa Chadema, Patrick Assenga kuomba mwongozo kwa Mwita ili ampe taarifa mjumbe wa CCM.

“Mwenyekiti hayo anayosema Mtinika hayapo katika hoja zilizoletwa mezani, hapaswi kuzungumzia Ilani ya CCM kwenye kikao hiki. Jiji hili linaongozwa na Ukawa. Sisi wajumbe wake hatupendi kuleta mambo ya vyama kwenye vikao kama hivi,” alisema Assenga ambaye ni diwani wa Tabata.

Mjumbe wa CCM, Abdallah Chaurembo ambaye ni Meya wa Temeke, alishangazwa na wajumbe wa Ukawa kwa kukataa wao wasitaje neno Ilani ya CCM .

“Nawashangaa sijui wanachopinga ni nini? Mapitio ya bajeti yameandaliwa kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ikiwa sambamba na Ilani ya CCM, chama tawala.

“Mkurugenzi nitakushangaa kama hutataja neno Ilani ya CCM katika makabrasha yako, kwa sababu nchi hii inaongozwa na Serikali inayotokana na chama tawala,” alisema Chaurembo.

Hoja ya Chaurembo ambaye ni diwani wa Charambe, ilimfanya mjumbe wa CUF ambaye ni Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kusimama na kumtaka mwenyekiti kufuata utaratibu wa kuendesha kikao hicho.

“Mwenyekiti naomba usimamie kikao hiki inavyotakiwa, naona unawaruhusu watu kujadili vitu ambavyo havipo. Ndiyo maana mara kwa mara tunaomba semina ya madiwani,” alisema Mtolea.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema wajumbe walionywa kuhusu kutoingiza mambo hayo kwenye vikao hivyo kwa kuwa jiji hilo linaendeshwa bila kujali itikadi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hilo, Sipora Liana alisema makadirio ya bajeti ilikuwa ni zaidi ya Sh13 bilioni, sehemu ya fedha hizo ni ruzuku kutoka Serikali Kuu na nyingine ni fedha za mapato ya ndani.